MASOMO YA MISA, APRILI 30 2023
DOMINIKA YA 4 YA PASAKA
JUMAPILI YA MCHUNGAJI MWEMA
MWANZO:
Zab. 33:5–6
Nchi imejaa fadhili za Bwana. Kwa neno la Bwana
mbingu zilifanyika, aleluya.
SOMO 1
Mdo 2:14, 36– 41
Siku ya Pentekoste Petro akasimama pamoja na
wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia,
Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya
kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyesulibisha kuwa Bwana na Kristo.
Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao,
wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia,
Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Krito, mpate kila mmoja kwa
jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha
Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na
kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na
kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile
wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 23:1 – 6 (K) 1
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa
na kitu.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)
Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa
mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
SOMO 2
1Pet. 2:20– 25
Kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu
ndio wema hasa mbele za Mungu. Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye
aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake.
Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana
kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa,
hakuogopfya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe
alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti; ili, tukiwa wafu kwa
mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.
Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na
Mwangalizi war oho zenu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yn. 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu
nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI
Yn. 10:1 – 10
Yesu aliwaambia Wayahudi, Amin, amin,
nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea
penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang’anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa
kondoo. Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita
kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Naye awatoapo kondoo humfuata,
kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa
maana hawazijui sauti za wageni.
Mithali hiyo Yesu aliwaambia; lakini wao
hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia.
Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin,
nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na
wanyang’anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa
mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe
na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo..
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment