MASOMO YA MISA, MEI 23, 2023
JUMANNE, JUMA LA 7 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 20 :17-27
Siku zile, toka Mileto Paulo alituma watu kwenda
Efeso, akawaita wazee wa kanisa. Walipofika
kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu
siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote,
nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi na majaribu
yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia
neno lo lote liwezalo kuwafaa, bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa
nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana
wetu Yesu Kristo.
Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda
Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;
isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba
vifungo na dhiki vyaningoja. Lakini
siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo
wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari njema ya
neema ya Mungu. Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote
niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena. Kwa
hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu
awaye yote. Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la
Mungu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 68 : 9-10, 19-20 (K) 32
K. Enyi falme wa dunia, mwimbieni Mungu. Au: K.
Aleluya.
Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema;
Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.
Kabila yako ilifanya kao lake huko;
Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.
(K)
Na ahimidiwe Bwana,
Siku kwa siku hutuchukulia mzigo wetu;
Mungu ndiye wokovu wetu.
Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa;
Na njia za kutoka mautini. (K)
SHANGILIO
Yn. 14:16
Aleluya, aleluya,
Nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine,
ili akae nanyi hata milele.
Aleluya.
INJILI
Yn. 17:1-11
Siku ile, Yesu aliinua macho yake kuelekea
mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako
naye akutukuze wewe. Kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili
kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue
wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza
duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.
Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa
utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. Jina lako
nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa
mimi, na neno lako wamelishika. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka
kwako. Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika
ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mimi
nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na
wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao.
Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment