MASOMO YA MISA, MEI 3, 2024
IJUMAA, JUMA LA 4 LA PASAKA
SIKUKUU YA WAT. FILIPO NA YAKOBO, MITUME
SOMO 1
1Kor. 15:1-8
Ndugu zangu, nawaarifu ile injili
niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo
mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini
bure.
Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale
niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu,
kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya
tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale
Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi
wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na
mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa
si kwa wakati wake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 19:1-4 (K) 4
(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
Usiku hutolea usiku maarifa. (K)
Hakuna lugha wala maneno,
Sauti yao haisikilikani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)
SHANGILIO
Yn. 14:6, 9
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi njia, na kweli na uzima, asema Bwana,
Filipo, aliyeniona mimi, amemweona Baba.
Aleluya.
INJILI
Yn. 14:8-14
Yesu alimwambia Tomasi: Mimi ndimi njia, na
kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua
mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.
Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba,
yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe
usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe
Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni
ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi
kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki
ya kwamba mimi ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo,
sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe.
Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi,
kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo
atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu,
hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina
langu, nitalifanya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment