MASOMO YA MISA, MEI 20, 2023
JUMAMOSI, JUMA LA 6 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 18:23-28
Paulo, akiisha kukaa Antiokia siku kadha wa
kadha aliondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji,
akiwathibitisha wanafunzi. Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzaliwa wa
Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko.
Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa
ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua
ubatizo wa Yohane tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila
na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi
zaidi.
Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya,
ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe; naye alipofika
akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu. Kwa maana
aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya
maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 47: 1-2, 7-9 (K) 7
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.
Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. (K)
Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)
Wakuu wa watu wamekusanyika,
Wawe watu wa Mungu wa Ibrahimu.
Maana ngao za dunia zina Mungu,
Ametukuka sana. (K)
SHANGILIO
Yn. 10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua,
nao wanifuata.
Aleluya.
INJILI
Yn. 16:23-28
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin,
amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa
hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.
Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambayo sitasema nanyi tena kwa
mithali; lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba. Na siku ile mtaomba kwa jina
langu; wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; kwa maana Baba
mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi
nalitoka kwa Baba. Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena
nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment