MASOMO YA MISA, MEI 19, 2023
IJUMAA, JUMA LA 6 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 18: 9-18
Bwana alimwambia Paulo kwa maono usiku,
Usiogope, bali nena, wala usinyamaze, kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana
mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji
huu. Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la
Mungu.
Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi
wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema,
Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria. Na Paulo
alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo
la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana
nanyi; bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni
ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo.
Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu.
Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha
hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu. Baada ya hayo Paulo
akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu;
na Prisila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko
Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 47:1-6 (K) 7
(K) Mungu ndiye mfalme wa dunia yote.
Au: Aleluya.
Enyi watu wote, pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe,
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. (K)
Atawatiisha watu wa nchi chini yetu,
Na mataifa chini ya miguu yetu.
Atatuchagulia urithi wetu,
Fahari ya Yakobo ambaye alimpenda. (K)
Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni;
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K)
SHANGILIO
Yn- 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema, nao walio wangu
nawajua, nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.
INJILI
Yn. 16:20-23
Siku ile Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Amin,
amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi
mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. Mwanamke azaapo, yuna
huzuni kwa kuwa saa yake imefika, lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena
ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni. Basi ninyi hivi
sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha
yenu hakuna awaondoleaye. Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin,
nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment