MASOMO YA MISA, MEI 18, 2023
ALHAMISI , JUMA LA 6 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 18 :1-8
Siku zile, Paulo alitoka Athene akafika
Korintho. Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzaliwa wa Ponto; naye
amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa
sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao; na
kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja,
kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema. Akatoa hoja zake katika sinagogi
kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.
Hata Sila na Timotheo walipotelemka kutoka
Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba
Yesu ni Kristo. Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung’uta mavazi
yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu
sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa. Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya
mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka
mmoja na sinagogi. Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na
nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98: 1-4 (K) 2
(K) Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa
mataifa: au: Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K)
SHANGILIO
Lk 24:25-26
Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia
katika utukufu wake.
Aleluya.
INJILI
Yn. 16: 16-20
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Bado
kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona. Basi
baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo
kidogo nanyi hamnioni na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? na hilo, Kwa
sababu naenda zangu kwa Baba? Basi walisema, neno gani hilo asemalo; hilo, Bado
kitambo kidogo? Hatujui asemalo.
Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza,
akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo kidogo
nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? Amin, amin,
nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi
mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
No comments:
Post a Comment