MASOMO YA MISA, MEI 15, 2023
JUMATATU, JUMA LA 6 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 16:11-15
Tuling’oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake
kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika
Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia
Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. Hata siku ya sabato
tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana
mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.
Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza
rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambave moyo
wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata
alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona
kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 149 :16, 9 (K) 4
(K) Bwana awaridhia watu wake. au Aleluya.
Au: Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)
Watauwa na waushangilic utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wote. (K)
SHANGILIO
Rum. 6 : 9
Aleluya, aleluya,
Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena
wala mauti haimtawali tena.
Aleluya.
INJILI
Yn. 15:26-16:4
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ajapo huyo
Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa
Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo
mmekuwapo pamoja nami.
Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa.
Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya
kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala
mimi. Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya
kuwa mimi naliwaambia.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment