Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, MEI 14, 2023


MASOMO YA MISA, MEI 14, 2023
DOMINIKA YA 6 YA PASAKA


MWANZO:
Isa. 48:20
Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amelikomboa taifa lake, aleluya.


SOMO 1
Mdo. 8:5-8, 14-17

Filipo alitelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifa- nya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na wratu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.

Na mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu, wakawapelekea Petro na Yohane; ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; Kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 66 :1-7, 16, 20, (K) 1

(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote, au: Aleluya.

Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake,
Tukuzeni sifa zake.
Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini! (K)

Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimbia jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu;
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. (K)

Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tulikomfurahia.
Atawala kwa uweza wake milele. (K)

Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu,
Wala kuniondolea fadhili zake. (K)



SOMO 2
1 Pet. 3 :15-18

Mwe tayari sikuzote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikrwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.

Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



SHANGILIO
Yn. 14:23

Aleluya, aleluya,
Yesu alisema: Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake. Aleluya.



INJILI
Yn. 14 :15-21

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.

Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai. Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu. Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment