Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, MEI 5, 2023


MASOMO YA MISA, MEI 5, 2023
IJUMAA, JUMA LA 4 LA PASAKA


SOMO 1
Mdo. 13:26-33

Paulo alisimama akawapungia mkono, akasema: Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe. Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu.

Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 2:6-11 (K) 7

(K) Ndiwe Mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
Au: Aleluya.

Nami nimemweka mfalme wangu
Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.
Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. (K)

Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
Utawaponda kwa fimbo ya chuma,
Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. (K)

Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili,
Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
Mtumikieni Bwana kwa kicho,
Shangilieni kwa kutetemeka. (K)


SHANGILIO
Yn. 20: 29

Aleluya, aleluya,
Wewe Toma, umesadiki kwa kuwa umeniona, wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.


INJILI
Yn. 14:1-6

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yngu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia, maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia.
Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?
Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment