NOVENA YA ROHO MTAKATIFU
SIKU YA PILI, JUMA MOSI
ROHO MTAKATIFU ANATUSAIDIA KUENEZA INJILI
“Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika utawala wa Mungu,” (Yn. 3:5).
Kanisa limepewa na Yesu ujumbe wa kuwaletea watu wote uzima mpya, uzima wa Mungu. Yesu aliwaambia mitume wake: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Nendeni basi mkawafanye watu wa makabila yote kuwa wafuasi wangu. Wabatizeni kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Wafundisheni kuyashika maagizo yote niliyowapeni. Nami nipo pamoja nanyi siku zote mpaka mwisho wa nyakati (Mt. 28: 18-20).
Sisi tuliobatizwa tumepata kuwa viungo vilivyo hai vya Mwili wa Fumbo wa Kristu; kwa Kipaimara tumeimarishwa na kuthibitishwa na Roho Mtakatifu. Tumekuwa taifa teule. Tumeshirikishwa ule ukuhani wa Kristu. Tumepokea ujumbe wa kueneza utawala wa Mungu.
Tunapopokea Sakramenti, na hasa ile Sakmenti ya Ekaristi, tunalisha imani na kuongeza mapendo, ambayo ni msingi wa utume wowote ule. Mapendo yanatuhimiza kueneza utawala wa Mungu na kumpenda Yesu Kristu aliyekuja kuwakomboa wanadamu wote.
Kila aliyebatizwa anao wajibu wa kueneza imani ya Mungu na utawala wake. Kwa hiyo tumuombe Roho Mtakatifu atuwezeshe kutimiza wito huo.
1. Ee Baba wa mbinguni
tunakuomba umpeleke Roho Mtakatifu aliangaze kanisa na kuliongoza, liweze
kuwafikishia mataifa yote habari njema ya wokovu.
W. Twakuomba utusikie
2. Ee Yesu Mkombozi wetu,
umtume Roho Mtakatifu awahimize wakristo wapate kutimiza wajibu wao wa kueneza
neno lako popote duniani
W. Twakuomba utusikie
3. Ewe Roho Mtakatifu Mfariji,
uamshe katika mioyo ya vijana wengi hamu ya kupenda kulitumikia kanisa lako na
kulihudumia taifa lako kwa u aminifu.
W. Twakuomba utusikie
4. Ewe mwanga wa mataifa,
uwajalie wanafunzi wasikie sauti yako mioyoni mwao, nawe unapowaita wasikose
kuisikia sauti yako, wawe tayari kujitoa kwa ajili ya ndugu zao.
W. Twakuomba utusikie.
5. Uwasaidie wazazi wawalee
vema watoto wao; uwatie moyo katika wito wao, wapate pia kuishiriki vema ile
kazi ya kueneza neno lako kwa jirani zao.
W. Twakuomba utusikie
6. Ewe Roho Mtakatifu,
uwasaidie wakristu wote kueneza habari njema ya wokovu, kwa sala, kwa sadaka na
kwa mifano ya maisha yao ya uchaji.
W. Twakuomba utusikie
7. Ewe mpaji wa mema, uwajalie
waumini mapaji yako saba, wasichoke kulieneza neno lako kwa hekima pasipo hofu.
W. Twakuomba utusikie.
TUOMBE:
Ee Mungu, unapenda watu wote waokoke, waifikie kweli yako. Tunakuomba
uwapeleke wafanyakazi walio wengi na wema katika shamba lako. Uwajalie
kulihubiri neno lako kwa imani kuu ili neno lako lienee na kupokewa na mataifa
yote, wapate nao kukujua wewe peke yako Mungu wao, Mungu wa kweli. Tunaomba
hayo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeliongoza kanisa lako sasa na milele.
W. Amina
No comments:
Post a Comment