“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Jumapili, Machi 26, 2023
Juma la 5 la Kwaresima
Eze 37: 12-14;
Zab 130: 1-8;
Rum 8: 8-11;
Yn 11: 1-45.
WATU WA UFUFUKO
Giza, na ukimya, vilifunika kifo kadiri ya tamadunii za Wayahudi. Ni vigumu
kupata maelezo kuhusu kutoharibika kwa roho au ufufuko wa wafu katika Agano la
Kale. Ayubu alisema “kuna matumaini kwa mti; kama ukikatwa unaweza kuchipua
tena, machipukizi mapya yatatokea tena. Lakini mwanadamu anavyokatwa, huanguka
chini na huvuta pumzi yake ya mwisho-atakuwa wapi? Maji ya bahari yanaweza
kutoweka, mito kukauka, lakini yule anayelala chini hawezi kuamka tena; mbingu
zitaisha kabla hajaamka, kabla hajaamka usingizini.” (Ayubu 14:7-12). Biblia
ilihifadhi kumbukumbu ya jinsi jambo lilivyokuwa gumu ili kutukumbusha ni kwa
jinsi ghani giza lilitisha katika kaburi, kabla ya ufufuko na mwanga wa Pasaka
duniani. Lakini pia mzaburi analeta matumaini. “Nijapopita katika giza la
mauti, sintaogopa mbaya, kwani wewe Bwana wa uhai utakuwa pamoja nami”
“Kifo” kinaonekana kutisha kwa watu wengi, lakini ni wazi kwamba hakuna
kitu tulicho na uhakika nacho katika maisha zaidi ya kifo. Wengi wetu
tunazungukwa na hofu, baada ya kifo kuna nini? Wafuasi hawakuwa na tofauti.
Hali yote inayo wazunguka inaonekana kutisha, na kwa upande mwingine Yesu
anatabiri kuwa kifo chake kipo karibu na kwa upande mwingine wanawaogopa
Wayahudi amabao walitaka kumpiga Yesu mawe mpaka afe. Kwa kipindi hichi tunaona
jibu laTomasi lilivyo na mashaka “twende na sisi tukafe pamoja naye”. Ni hakika
kwamba hofu ya kifo iliwakumba wafuasi. Yesu kwa kumfufua Lazaro kutoka wafu
anataka kuwafunulia mitume na watu wengine kwamba yeye ni nani “YEYE NI UFUFUO
NA UZIMA”.
Kifo ni nini?
Katika Injili ya leo, Yesu anakwepa kutumia neno ‘kufa’ badala yake
anatumia ‘kupumzika’ akionesha kifo cha Lazaro. Kifo kilionekana kuwa ni kitu
hasi na pia mwisho wa kitu. Lakini Yesu kwa kutumia neno “kupumzika’ anataka
kuwaambia wafuasi kwamba kifo sio mwisho wa kila kitu, bali njia ya kupitia
kutoka hali moja kwenda hali nyingine ya maisha. Kifo ni njia ya kupitia kutoka
maisha haya ya duniani kuelekea maisha ya milele, njia ambayo imefunguliwa kwa
ufufuko wa Yesu.
Ufufuko ni nini?
Wayahudi waliamini kwamba ni Mungu mwenyewe anaweza kurudisha uhai. Yesu
anatumia kifo cha Lazaro kuonesha kweli yeye ni mwana wa Mungu, kwa kumfufua
kutoka wafu. Lazaro ambaye alikuwa amekufa kwa siku nne, sasa anakuwa hai.
Lazaro aliyekuwa amekufa sasa anatembea kutoka kaburini. Wayahudi waliamini
kuhusu ufufuo wa wafu lakini ilikuwa mpaka dunia itakapopita. Na hapa wanaona
kitu ambacho kina washangaza, mtu ambaye alikuwa amekufa kwa siku nne, anakuwa
hai tena. Walio shuhudia waliamini kabisa Yesu sio nabii wa kawaida wala
mwalimu wa kawaida bali Mungu mwenyewe. Yesu anaendelea kuonesha kwamba ufufuko
sio tukio baada ya kifo, bali linaanza duniani kwa kuishi ukiwa umeunganika na
Yesu.
Katika somo la kwanza katika kitabu cha nabii Ezekieli, anatangaza tukio
ambalo Mungu anaenda kulitenda, muujiza wa ajabu. Mungu analeta uhai katika
mifupa iliokauka. Mungu atafunua makaburi ambayo walikuwa wamefungwa,
atawafanya watoke katika makaburi yao na kuwaongoza tena katika Nchi yao. Roho
wa Mungu aliingia kila mahali na maisha yakaanza. Yalianza wakati wa mwanzo wa
dunia, wakati Mungu anamuumba mwanadamu kutoka mavumbini, alimpulizia pumzi ya
uhai na mwanadamu akaishi (Mwa 2:7). Hakuna kinacho shindikana kwa Roho wa
Mungu. Anaweza kuleta maisha pia hata katika mifupa iliyo kauka kabisa.
Katika somo la pili, Paulo anatuambia, Yesu akiwa mtu kama sisi, alikufa.
Lakini alifufuka. Yesu ana Roho kamili wa Mungu, ni kwamba ana ndani yake uhai
wa Kimungu ambao hauwezi kufa. Yesu alikuwa na uhai huu wa Kimungu ndani yake.
Roho wa Mungu alimfufua, na kumtambulisha katika utukufu wa Baba. Wale walio
batizwa katika roho wake, katika maisha yake, hawafi tena. Maisha yetu katika
ulimwengu huu yataisha, yatafika mwisho, lakini haitakuwa mwisho wa kila kitu.
Roho aliye mfufua Yesu atatufua na kuipatia uzima wa milele miili Yetu inayo
kufa.
Mkristo haamini katika kifo na ufufuko kama kitu ambacho kitatokea mwisho
wa dunia. Ana amini kwamba mtu aliyekombolewa na Yesu hafi. Yesu alitangaza kwa
Martha kwamba “kila anaye niamini mimi hatakufa kamwe”(Mtari wa 26). Pasaka
inakaribia ni majuma mawili tu yajayo, na waliyo wengi tunatazama ufuko kama
tukio litakalo tokea baadae. Tunashindwa kuishi kama watu wa ufufuko. Kwaresima
inaonekana kama maombolezo, kujinyima, toba, lakini kwa hakika kwaresima ni
kipindi cha kujifunza jinsi ya kuishi maisha ya ufufuko. Yesu amekuja
kutukomboa sisi, sio tu baada ya kifo chetu bali pia tukiwa hai. Tukiwa na
matumaini na tukiishi Imani katika ufufuko tuishi kama watu wa ufufuko kuanzia
leo. Na yeye aliyempa Lazaro uhai kwa hakika atatupa sisi uhai, uhai tele.
Sala: Bwana, wewe ni ufufuo na uzima. Nisaidie niondokane a muonekano wangu
mbaya kuhusu uzima na kifo. Ninaomba nikuwe katika Imani ya roho wa uzima aliye
ndani mwangu. Ninakuomba niweze kutambua Uzima wa Kimungu ndani mwangu.
Ninaomba nitoke katika hofu zangu, na kwenda katika maisha ya ufufuo. Yesu,
nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment