MASOMO YA MISA, MACHI 26, 2023
DOMINIKA YA 5 YA KWARESIMA
MWANZO:
Zab. 43:1 – 2
Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo
haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe ndiwe Mungu uliye nguvu
zangu.
SOMO 1
Eze. 37:12 – 14
Bwana Mungu asema hivi; Tazama, nitafunua
makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu,
nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi
Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu,
enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami
nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo,
na kuyatimiza asema Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza asema Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 130 (K) 7
(K) Kwa Bwana kuna fadhili, na kwake kuna ukombozi
mwingi.
Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia,
Bwana, uisikie sauti yangu.
Masikio yako na yaisikilize
Sauti ya dua zangu. (K)
Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?
Lakini kwako kuna msamaha,
Ili Wewe uogopwe. (K)
Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja,
Na neno lake nimelitumainia.
Nafsi yangu inamngoja Bwana,
Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
Naam, walinzi waingojao asubuhi.
Ee Israeli, umtarajie Bwana. (K)
Maana kwa Bwana kuna fadhili,
Na kwake kuna ukombozi mwingi.
Yeye atamkomboa Israeli
Na maovu yake yote. (K)
SOMO 2
Rum. 8:8 – 11
Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.
Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali
mwaifuata roho.
Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa
Kristo, huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu
ya dhambi; bali roho yenu I hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho wake
yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo
Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho
wake anayekaa ndani yenu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yn. 11:25, 26
Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima, asema Bwana;
Yeye aniaminiye mimi, hatakufa kabisa hata milele.
INJILI
Yn. 11:1 – 45
Basi mtu mmoja alikuwa hawezi, Lazaro wa
Bethania, mwenyeji wa mji wa Mariamu na Martha, dada yake. Ndiye Mariamu yule
aliyempaka Bwana marhamu, akamfuta miguu kwa nywele zake, ambaye Lazaro nduguye
alikuwa hawezi.
Basi wale waumbu wakatuma ujumbe kwake wakesema,
Bwana, yeye umpendaye hawezi. Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa
mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa
huo. Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake na Lazaro. Basi aliposikia ya
kwamba hawezi, alikaa bado siku mbili pale pale alipokuwapo. Kisha, baada ya
hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena.
Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu
Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena? Yesu
akajibu, Je! Saa za mchana si kumi na mbili? mtu akienda mchana hajikwai; kwa
sababu aiona nuru ya ulimwengu huu. Basi akienda usiku hujikwaa; kwa sababu
nuru haimo ndani yake.
Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo,
akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha.
Basi wale wanafunzi wakamwambia, Bwana, ikiwa amelala, atapona. Lakini Yesu
alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhani aya kuwa ananena habari ya
kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazro amekufa. Nami
nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwapo huko, ili mpate kuamini; lakini na
twendeni kwake. Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe,
Twendeni na sisi ili tufe pamoja naye.
Basi Yesu alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo
kaburini yapata siku nne. Na Bethania ilikuwa karibu na Yerusalemu, kadiri
ya maili mbili hivi; na watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha
na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao.
Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja,
alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia
Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa
najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu
yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku
ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye
mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa
kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi
nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.
Naye alipokwisha kusema hayo, alikwenda zake;
akamwita umbu lake Mariamu faraghani, akisema, Mwalimu yupo anakuita. Naye
aliposikia, aliondoka upesi, akamwendea. Na Yesu alikuwa hajafika ndani ya
kijiji; lakini alikuwa akalipo pale pale alipomlaki Martha. Basi wale Wayahudi
waliokuwapo na Mariamu nyumbani, wakimfariji, walipomwona jinsi alivyoondoka
upesi na kutoka, walimfuata; huku wakidhania ya kuwa anakwenda kaburini ili
alie huko.
Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na
kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa,
ndugu yangu hangalikufa. Basi Yesu alipomwona Analia, na wale Wayahudi
waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake, akasema,
Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame. Yesu akalia machozi. Basi
Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda. Bali wengine wao wakasema, Je!
Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hawezi kumfanya na huyu asife? Basi Yesu
hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango,
na jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa;
maana amekuwa maiti siku nne. Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba
ukiamini utauona utukufu wa Mungu? Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua
macho yake juu, akasema, Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya
kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria
nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.
Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu,
Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na
mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia Mfungueni, mkamwache
aende zake.
Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa
Mariamu, na kuyaona yale aliyoyafanya, wakamwamini.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment