Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

UHURU KWA NDANI YA KRISTO!


“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Jumatano, Machi 29, 2023
Juma la 5 la Kwaresima

Dan 3: 14-20, 24-25, 28;
Dan 3: 52-56;
Yn 8: 31-42.


UHURU KWA NDANI YA KRISTO!


Uhuru ni kitu ambacho kina thaminiwa na wote. Uhuru wa kweli ni muhimu kwa utu wa binadamu na ni katika uhuru mtu anaweza kujiongoza mwenyewe kwenda kwenye wema. Ni alama isio pingika ya Kimungu ndani mwetu. Lakini kwa kweli, uhuru unaeleweka vibaya kwa kudhani kwamba ni kufanya chochote ambacho mtu anapenda kufanya. Maovu mengi, ukandamizaji, na uonevu unafanywa chini ya jina la uhuru, na wale walio wema wanateseka katika hali mbali mbali ya utumwa. Katika hali ya kweli, ni uwezo wa kuchagua kile kilicho chema zaidi. 

Katika somo la kwanza, tunaona hali mbili za utumwa. Tunaona jinsi Danieli anateseka juu ya utumwa wa nje, kwasababu ya uonevu wa mfalme, wakati mfalme na viongozi wake wanateseka ndani kwasababu ya utumwa wa dhambi. Wakati huo huo tunaona uhuru wa ndani wa Danieli na jamaa wake. 
Pamoja na kwamba walikuwa wamefungwa waliwekwa huru kufanya mapenzi ya Mungu. Uhuru huu unatokana na kujitoa kwao kwenye ukweli wa Kimungu na uwepo wa nguvu ya Mungu. 
Je, unataka kuwa huru? Katika hali ya akili ya kawaida hili ni jibu la kawaida kujibu. Lakini katika hali ya kuishi hili, ni swali ngumu kulijibu. Watu wengi wanajisikia vizuri kuishi kwenye dhambi. Dhambi inaleta kuridhika kwa uongo ambapo inakuwa vigumu kuacha. Dhambi inaweza kukufanya ujisikie vizuri kwa muda, ingawaje madhara yake makubwa yanakunyima uhuru na furaha. Kwahiyo, je unataka kuwa huru kuishi kama mtoto wa Mungu aliye juu? Kama unajibu “ndio” jiandae kuumia, lakini katika hali ya kuelekea kwenye uhuru wa kweli. 

Kuacha dhambi inahitaji kujitakasa. Hali ya “kuiachia dhambi iondoke” inahitaji sadaka na majitoleo. Inakuhitaji wewe kujiaminisha kwa Mungu katika kweli na kuacha. Kwakufanya hivyo, unahisi hali flani ya kifo ndani mwako, kwa hisia zako mwenyewe na kwa mapenzi yako mwenyewe. Hili, linaumiza, lakini katika hali ya kuanguka kwa ubinadamu. Lakini hili ni kama kufanyiwa upasuaji ambao unalenga kutoa ugonjwa fulani ndani ya mwili. Upasuaji huu unaweza kuwa unauma, lakini ndio njia pekee ya kuondoa ugonjwa huo usikuumize. Yesu ndiye mganga wa Kimungu wa upasuaji na jinsi anavyokuweka huru ni kwa njia ya mateso na kifo chake. Kifo cha Yesu msalabani kilileta uhai Ulimwenguni.

Kipindi cha kwaresima ni kipindi zaidi ya kipindi kingine kile, ambacho unapaswa kiingia ndani kabisa na kutambua dhambi yako, kwa malengo ya kutambua ni yapi yanayo kushikilia kwenye dhambi. Ili uweze kumkaribisha Daktari wa Kimungu kusafisha vidonda vyako na kuvitibu na kuleta uponyaji. Usikubali kwaresima iishe kabla hujachunguza dhamiri yako katika kweli, na kuungama dhambi zako kwa moyo wako wote. Mungu anataka wewe uwe huru! Tamani hali hii wewe mweyewe na anza na hali ya kujitakasa ili uweze kuachilia mizigo yako mikubwa. 

Sala: Bwana, ninatamani kuwa huru kutoka katika dhambi zangu zote ili niweze kuishi huru kama mtoto wako. Nisaidie Bwana wangu, kukabili dhambi zangu katika kweli na uwazi. Nipe ujasiri niweze kuzikiri katika sakramenti ya kitubio, ili niweze kushangilia kwa yote ulioweka ndani mwangu kwa njia ya mateso na kifo chako. Yesu, nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment