MASOMO
YA MISA MACHI 29, 2023
JUMATANO, JUMA LA 5 LA KWARESIMA
SOMO 1
Dan. 3:14-20, 24-25, 28
Nabukadreza, aliwaambia, Enyi Shadraka, na
Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala
kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari
wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na
santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu
niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika
tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono
yangu?
Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego,
wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hatuna haja kukujibu katika neno
hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tnayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile
iwakayo moto; naye atatuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na
mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi
hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu
uliyoisimamisha.
Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya
uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri
watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha
akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na
Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa
haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali
wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme.
Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea
katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wan ne ni mfano wa mwana
wa miungu.
Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu
wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa
watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao
ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Dan. 3:52-56 (K) 52
(K) Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;
Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)
Umehimidiwa katiak hekalu la fahari yako
takatifu;
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)
Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya
makerubi;
Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 11:25, 26
Mimi ndimi ufufuo na uzima, asema Bwana, yeye
aniaminiye, hatakufa hata milele.
INJILI
Yn. 8:31-42
Yesu aliwaambia wale Wayahudi waliomwamini.
Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena
mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.
Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala
hatujawa watumwa wa mtu wakati wowote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?
Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila
atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana
hukaa sikuzote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya
kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu; lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu
halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo
mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo.
Wakajibu, wakamwambia, Baba yetu ndiye Ibrahimu!
Yesu akawaambia, Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake
Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo
kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi
za baba yenu.
Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa
zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani Mungu. Yesu akwaambia, Kama Mungu angekuwa
baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala
sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment