MASOMO
YA MISA, MACHI 28, 2023
JUMANNE, JUMA LA 5 LA KWARESIMA
SOMO 1
Hes. 21:4-9
Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya
Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu watu wakafa moyo kwa sababu ya
ile njia. Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka
nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na
roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.
Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu,
wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi
kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee
nyoka hawa. Basi, Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka
ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo,
ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka
amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab.
102:1-2, 15-20 (K) 1
(K) Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, kilio changu
kikufikie.
Ee Bwana, usikie kuomba kwangu,
Kilio change kikufikie,
Usinifiche uso wako siku ya shida yangu,
Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.
(K)
Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
Atakapoonekana katika utukufu wake,
Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
Asiyadharau maombi yao. (K)
Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,
Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)
SHANGILIO
Yn. 8:12
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye
anifuataye, atakuwa na nuru ya uzima.
INJILI
Yn. 8:21-30
Yesu aliwaambia Mafarisayo: Mimi naondoka, nanyi
mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi
kuja.
Basi, Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa
asema, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja?
Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu;
ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya
kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye,
mtakufa katika dhambi zenu.
Basi wakamwambia, U nani wewe? Yesu akawaambia,
Hasa neno lilo hilo ninalowaambia. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu;
lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake ndiyo ninenayo
katika ulimwengu.
Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba. Basi
Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo
mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila
kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami;
hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo.
Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamwini.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment