MASOMO YA MISA, APRILI 19, 2023
JUMATANO, JUMA LA 2 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo 5:17-26
Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja
naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu,wakawakamata
mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya
gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu
maneno yote ya Uzima huu. Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza
kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu
wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete.
Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari,
wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya
mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani. Basi jemadari wa hekalu na
wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao,
litakuwaje jambo hilo. Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale
mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu. Ndipo
yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa
maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 34:1-8
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.
Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi. (K)
Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)
Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
Malaika wa Bwana hufanya kituo,
Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini. (K)
SHANGILIO
Rum. 6:9
Aleluya, aleluya,
Kristo akiisha kufufuka, katika wafu hafi tena.
Mauti haimtawali tena.
Aleluya.
INJILI
Yn 3:16-21
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu,
hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima
wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali
ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini
amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Na
hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza
kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye
mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.
Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya
kuwa yametendwa katika Mungu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment