MASOMO YA MISA, APRILI 13, 2023
OKTAVA YA PASAKA, ALHAMISI
SOMO 1
Mdo 3:11-26
Siku zile, kiwete yule aliyeponywa alipokuwa
akiwashika Petro na Yohane, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile
lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana. Hata Petro alipoyaona haya
akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona
mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi,
au kwa utauwa wetu sisi? Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa
baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana
mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana
yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa
uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Na kwa
imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua;
na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu
ninyi nyote. Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua
kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu
tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa,
ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja
nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu
mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za
kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake
watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu. Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba,
Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni
yeye katika mambo yote atakayonena nanyi. Na itakuwa ya kwamba kila mtu
asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake. Naam, na
manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena,
walihubiri habari za siku hizi. Ninyi mmekuwa watoto wa manabii na wa maagano
yale, ambayo Mungu aliagana na baba zenu, akimwambia Ibrahimu, Katika uzao wako
kabila zote za ulimwengu zitabarikiwa. Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake
Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja
wenu na maovu yake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 8:1, 4-8
(K)Ee, Mungu, Bwana wetu; jinsi lilivyo tukufu
jna lako duniani mwote.
Wewe, Mungu, Bwana wetu
Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie? (K)
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake. (K)
Kondoo, na ng'ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni;
Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitacho njia za baharini. (K)
INJILI
Lk 24:35-48
Wanafunzi waliwapa habari ya mambo yale ya
njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.
Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye
mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu.
Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba
wanaona roho. Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni
mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe.
Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona
mimi kuwa nayo. Na baada ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake.
Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna
chakula cho chote hapa? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala
mbele yao.
Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu
niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe
yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi. Ndipo
akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo
ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba
mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi,
kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment