MASOMO YA MISA, APRILI 6, 2023
ALHAMISI KUU
SOMO 1
Kut 12:1-8, 11-14
Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya
Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa
kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya
kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba
zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache
kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na
watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa
kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo
wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika
mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko
lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.Nao watatwaa baadhi ya damu yake
na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba
watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate
usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Tena mtamla hivi; mtakuwa
mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi
mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. Maana nitapita kati ya nchi
ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya
Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya
Misri; Mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba
mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo
lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa
ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu
katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 116:12-13, 15-18
(K)Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je,
!Si ushirika wa damu ya Kristo?
Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana. (K)
Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako,
Umevifungua vifungo vyangu. (K)
Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote. (K)
SOMO 2
1Kor 11:23-26
Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa
nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha
kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni
hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe,
akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila
mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe
hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
INJILI
Yn 13:1-15
Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali
akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba,
naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati wa
chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni
Iskariote, moyo wa kumsaliti; Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote
mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu,
aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga
kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu,
na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo
akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia,
Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe
hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika
nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu
na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya
kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote.
Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi.
Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena,
akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na,
Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana
na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.
Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.
Injili ya Bwana.........Sifa Kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment