“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Alhamisi, Aprili 6, 2023
Juma Kuu
ALHAMISI KUU
Kut 12: 1-8,11-14;
Zab116: 12-13,15-18;
1 Kor: 11:23-26;
Yn 13: 1-15
FANYENI HIVI KWA KUNIKUMBUKA MIMI!
Leo tunaanza siku tatu, muhimu katika Pasaka-maadhimisho matatu makuu ya
Imani yetu Katoliki. Leo tunaanza na zawadi ya Bwana wetu ya Ekaristi Takatifu
tuliopewa kwa ukuhani aliosimika. Kesho tunaingia katika fumbo la Msalaba. Na
Jumamosi jioni tunaingia katika utukufu wa ufufuko wake.
Alhamisi kuu jioni, tuna adhimisha siku ambayo Yesu aliweka Ekaristi
Takatifu, kwa kusema “fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” Tangu siku hiyo Misa
Takatifu imekuwa ikiadhimishwa mara nyingi sana katika kila pembe ya dunia kwa
kutii amri ya Yesu.
Kama tungeelewa thamani na zawadi hii Takatifu, Ekaristi Takatifu! Ekaristi
Takatifu ni Mungu mwenyewe katika ulimwengu huu, tuliopewa sisi kutugeuza na
kutufanya tuwe tunachopokea. Ekaristi Takatifu katika ukweli halisi,
inatubadilisha sisi tuwe kama Kristo mwenyewe. Tukipokea Ekaristi Takatifu
tunavutwa kwenye maisha ya Kimungu ya Utatu Mtakatifu. Tunaungana na Mungu na
tunapewa chakula cha uzima wa milele.
Yesu pia alioonesha mfano wa unyenyekevu wa hali ya juu na huduma ambayo tunapaswa
kuitoa na kuiiga tunapo amua kumfuata na kuwa wamoja pamoja naye. Aliwaosha
miguu mitume ili kuwafundisha wao na sisi kwamba mwili na damu yake tumepewa
ili tuweze kupenda kama yeye alivyo penda. Ekaristi inatugeuza kuwa watumishi
wa unyenyekevu wa kweli. Tunaitwa tuwahudumie ndugu zetu. Huduma hii inachukua
hali mbali mbali lakini ndicho tulichoitiwa kufanya. Huduma katika unyenyekevu
ni muonekano mzuri wa kueleza muunganiko wetu na Mwana wa Mungu. Ukuu
unaonekana katika hali ya dunia kama kitu kizuri na cha kutamanika. Lakini leo
Yesu anatupa aina nyingine ya ukuu. Alhamisi kuu, anaonesha kwamba ukuu huu
katika unyenyekevu unapatikana katika huduma hii. Ili kumuiga yeye inatupasa
kuacha majivuno yetu kwanza. Na hili linawezekana tunapopokea Ekaristi Takatifu
tukiwa safi na wenye Imani. Ekaristi inatusaidia kuwapenda na kuwatumikia namna
hii. Na kitendo hichi cha upendo na huduma kitashinda katika mioyo yetu kwa
ajili ya Ufalme wa Mungu. Tukiwa tuna adhimisha Alhamisi kuu, tunapata
changamoto ya kuangalia unyenyekevu wetu, na kubadilika na kujikita katika
kuwahudumia wengine.
Juu ya Msalaba, alitoa maisha yake kwasababu ya dhambi zetu na
kutupatanisha na Baba. Lakini kifo chake msalabani haina maana kwamba
tutakwenda Mbinguni moja kwa moja. Tunapaswa kushirikiana na neema yake aliotoa
pale msalabani. Na hii ndio Ekaristi iliotoka ndani yake. Yesu aliyekufa juu ya
Msalaba ndiye Yesu yule yule aliye aliye juu ya altare wakati wa misa. Ambaye
alilipia dhambi zetu pale msalabani ndiye yule yule anaye tupa neema zake na
ukombozi juu ya altare wakati wa misa. Juu ya Msalaba Yesu alitoa sadaka kamili
ambayo haina haja ya kurudiwa tena. Katika altare sadaka ile ile ya Yesu
alioitoa inawekwa wazi tena kwa ajili ya ukombozi wetu. Si kwamba inarudiwa
tena bali ni sadaka ile ile ya Yesu alioitoa msalabani. Inawezekana je? Ni
kwasababu Mungu hafungwi na sehemu wala wakati wala historia, ndio maana sadaka
inakuwa ileile. Yeye anayafanya yaliotokea wakati ule yawe tena wazi juu ya
altare. Kwahiyo juu ya altare anatupa tena nguvu ya kukabili madimbwi ya dhambi
na kuingia katika uwepo wake katika hali kamili. Kwa hiyo, kilicho tokea pale
msalabani ndicho kinacho tokea altareni.
Ndivyo Yesu alivyo jikita katika kuleta ufalme wake kwetu. Hivyo, tutakavyo
kwenda kanisani leo, tuangalie kwa makini katika hostia Takatifu na kumuona
Yesu akiwa mbele yetu. Na kumuona yeye akitupa huruma yake. Tumuone yeye akitoa
upendo wake.
Sala: Bwana, nisaidie niweze kuwaza jinsi ya kuwa mtumishi. Nisaidie niweze
kuishi unyenyekevu huu kwa matendo yangu. Ninaomba zawadi ya mwili wako
Mtakatifu na damu yako vinibadilishe niweze kuwa mtu yule ambaye unapenda niwe.
Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment