“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumatatu, Aprili 10, 2023
Oktava ya Pasaka
Mdo 2:14,22-32
Zab 16:1-2,5-11
Mt 28:8-15.
KUMWABUDU BWANA MFUFUKA!
Habari kuhusu Yesu mfufuka zinaleta hali mbili kwa wale wanaosikia kuhusu
habari hii hapo kwanza. Moja ni muelekeo wa kumfuata Yesu mfufuka na nyingine
ni muelekeo wa kukataa kuhusu Yesu mfufuka. Wakati wakina Maria na wenzao
walikuwa na furaha ya kutangaza habari hii njema ya ufufuko, viongozi wa
Wawayahudi wanahofu na wanaogopa kuhusu kukiri na kukubali habari hizi. Wakati
wakina Maria wanatafuta kila njia na namna ya kumweleza kila mtu kuhusu habari
hii njema ya ufufuko wa Bwana, Viongozi wa Wayahudi wanatafuta njia ya kuificha
habari hii njema isienee kwa kwa watu.
Leo ni siku ya pili katika oktava ya Pasaka. Ina maana kwamba leo ni
Pasaka. Tunasherekea siku ya Pasaka kwa mfululizo wa siku nane na kuingia
katika jumapili ya Huruma ya Mungu. Hivyo siku hizi nane ni siku ambazo
tunapaswa kubaki na kutafakari kwa undani kabisa na kuhisi kama hawa wanawake
watakatifu baada ya kutambua kwamba Yesu hayupo tena kaburini amefufuka.
Tunapaswa kujiachia wenyewe tuingie kwenye mafumbo ya ufufuko. Tunapaswa kuyaona
kama yalivyo. Tunapaswa tutazame zawadi hii, na mshangao wa hakika wa ufufuko,
Yesu ameangamiza matokeo ya dhambi. Aliangamiza kifo chenyewe.
Wakati hawa wanawake wakitoka kaburini, maandiko yanatuambia kwamba
walikutana na Yesu mfufuka wakiwa njiani. Na yanasema kwamba walimuona Yesu, na
walimkaribia na kuishika miguu yake, na kumwabudu”. Hili sio tendo dogo la
kuabudu na upendo. Kitendo hichi cha kumtukuza na kumwabudu Yesu kinaonesha
kwamba hawaku muamini tu, bali walimwabudu. Tunapaswa kufanya hivyo, kama wao.
Tutumie muda huu wa Oktava ya Pasaka na kutafakari juu ya ufufuko na kuwa
na muda juu ya unyenyekevu wa kumwabudu Yesu. Tujiachie wenyewe tuje mbele ya
Yesu uso kwa uso, na kumwacha yeye mwenyewe abadilishe maisha yako.
Sala: Bwana, nina amini. Nina amini kwamba umefufuka kwa ushindi juu ya
dhambi. Ninakuomba unisadie kuelewa na kuhisi hali hii ya utukufu wa ajabu
katika maisha yangu. Ninakuabudu kwa upendo usio pimika, Bwana mpendwa.
Nisaidie nikuabudu wewe kwa hali yangu yote. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki:
see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment