MASOMO YA MISA, FEBRUARI 21, 2026
JUMAMOSI BAADA YA MAJIVU
SOMO 1
Isa. 58:9-14
Bwana asema hivi: Kama ukiiondoa nira; isiwepo
kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu
mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako
itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.
Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi
yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama
bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.
Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa
ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza
mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia.
Kama ukigeuza mguu wako usiihalifu sabato,
usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na
siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako
mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo
utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi
palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana
kimenena hayo.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 86:1-2, 3-4, 5-6 (K) 11
(K) Ee Bwana, unifundishe njia yako;
Nitakwenda katika kweli yako.
Nitakwenda katika kweli yako.
Ee Bwana, utege sikio lako unijibu,
Maana mimi ni maskini na mhitaji,
Unihifadhi nafsi yangu,
Maana mimi ni mcha Mungu.
Wewe uliye Mungu wangu,
Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini. (K)
Wewe, Bwana, unifadhili,
Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe, Bwana. (K)
Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe,
Na mwingi wa fadhili,
Kw awatu wote wakuitao.
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu. (K)
SHANGILIO
Eze. 33:11
Waambie, kama mimi niishivyo, asema Bwana Mungu,
Sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; Bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake
akaishi.
INJILI
Lk. 5:27-32
Siku ile: Yesu akaona mtoza ushuru, jina lake
Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha vyote, akaondoka,
akamfuata.
Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake;
palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi
chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unukia
wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na
wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu,
isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate
kutubu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment