MASOMO YA MISA, MACHI 19, 2023
DOMINIKA YA 4 YA KWARESIMA
MWANZO
Isa. 66:10 – 11
Furahi, Jerusalemu, mshangilieni ninyi nyote
mmpendao; furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na
kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake.
SOMO 1
1Sam. 16:1, 6-7, 10-13
Bwana akamwambia Samweli, Ijaze pembe yako
mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia
mfalme katika wanawe.
Ikawa walipokuja, Samweli alimtazama Eliabu,
akasema, Yakini masihi wa Bwana yupo hapa mbele zake. Lakini Bwana akamwambia
Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi
nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama
sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.
Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli,
Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia
Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama,
anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa
sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao.
Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbu lake lilikuwa la kupendeza.
Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.
Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta,
akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu
tangu siku ile.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
ZAB. 23 (K) 1
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa
na kitu.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza. (K)
Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa
mauti,
Sitaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
SOMO 2
Efe. 5:8 – 14
Zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa
nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru; Kwa kuwa tunda la nuru ni
katika wema wote na haki na kweli; mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. Wala
msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; kwa kuwa
yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. Lakini yote yaliyokemewa
hudhihirishwa na nuru; maana kila kilichodhihirika ni nuru. Hivyo husema, Amka
wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yn. 8:12
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye
anifuataye atakuwa na nuru ya uzima.
INJILI
Yn. 9:1 – 41
Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu
tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda
dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, Huyu
hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani
yake. Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana; usiku
waja asipoweza mtu kufanya kazi. Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya
ulimwengu.
Alipokwisha kusema hayo alitema mate chini,
akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho, akamwambia, Nenda
kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na
kunawa; akarudi anaona.
Basi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa
ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La; lakini amefanana naye. Yeye
mwenyewe alisema, Mimi ndiye.
Basi wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje?
Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia,
Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, naikapata kuona. Wakamwambia
Yuko wapi huyo? Akasema, Mimi sijui.
Basi wakampeleka kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu
zamani. Nayo ilikuwa sabato, hapo Yesu alipofanya zile tope na kumfumbua macho.
Basi Mafarisayo nao wakawmuliza tena jinasi gani alivyopata kuona. Akawaambia,
Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona. Basi baadhi ya
Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato.
Wengine wakasema, Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo? Kukawa
matengano kati yao. Basi wakamwambia yule kipofu mara ya pili, Wewe wasemaje
katika habari zake kwa vile alivyokufumbua macho? Akasema, Ni nabii.
Basi Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa
alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hata walipowaita wazazi wake yule
aliyepata kuona. Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema
kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa? Wazazi wake wakawajibu,
wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu;
lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho.
Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe. Wazazi wake
waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayaahudi walikuwa
wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na
sinagogi. Ndiyo sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye.
Basi mara ya pili wakamwita yule mtu aliyekuwa
kipofu, wakamwambia, Mpe Mungu utukufu. Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye
dhambi. Basi yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno
moja, kuwa mimi nilikuwa kipofu na sasa naona. Basi wakamwambia, Alitutendea
nini? Alikufumbua macho jinsi gani? Akawajibu, Nimekwisha kuwaambia, wala
hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi
wake? Basi wakamshutumu, wakasema, Wewe u mwanafunzi wake yule; sisi tu
wanafunzi wa Musa. Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule
hatujui atokako. Yule mtu akajibu, akawaambia, Hili ni ajabu! Kwamba ninyi
hamjui atokako, naye alinifumbua macho! Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye
dhambi; bali mtu akiwa mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake; humsikia huyo.
Tokea hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye
alizaliwa hali hiyo. Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno
lolote.
Wakajibu, wakamwambia, Ama! Wewe ulizaliwa
katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa nje. Yesu akasikia kwamba
wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu? Naye
akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini? Yesu akamwambia, Umemwona,
naye anayesema nawe ndiye. Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia.
Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa
hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu. Baadhi ya Mafarisayo
waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?
Yesu akamwambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa
mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment