MASOMO YA MISA, MACHI 25, 2023
JUMAMOSI JUMA LA 4 LA KWARESIMA
SHEREHE YA KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA
SOMO 1
Isa. 7:10 – 14
Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara
ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali
palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye
akasema, Sikilizeni sana, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu
kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana
mwenyewe atawapa ishara. Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto
mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 40:6 – 10 (K) 7 , 8
(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya
mapenzi yako.
Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)
Katika gombo la chuo nimeandikiwa
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko
kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa. (K)
SOMO 2
Ebr. 10:4 – 10
Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa
dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili
uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye
mapenzi yako, Mungu.
Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka
za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo
kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi
yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo
tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yn. 1:14
Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi
tukaona utukufu wake.
INJILI
Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na
Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira
aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake
bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa
neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake,
akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope,
Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa
mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana
wa Aliye ju, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.
Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.
Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika
akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu
zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa
kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua
mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye
aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema,
Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika
akaondoka akaenda zake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment