MASOMO YA MISA, MACHI 16, 2023
ALHAMISI, JUMA
LA 3 LA KWARESIMA
SOMO 1
Yer. 7:23-28
Naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni
sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika
njia ile yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala
kutega sikio lao, bali walikwenda kw amashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa
mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu
walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote
manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku na kuwatuma. Lakini
hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu;
walitenda mabaya kuliko baba zao. Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini
hawatakusikiliza; nawe utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, Taifa
hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho;
uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali vinywa vyao.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 95:1-2, 6-9 (K) 7
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu.
Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi. (K)
Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K)
Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
SHANGILIO
Zab. 51:10, 12
Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Unirudishie furaha ya wokovu wako.
Unirudishie furaha ya wokovu wako.
INJILI
Lk. 11:14-23
Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo
alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, Atoa
pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo
mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe
kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa
Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa
ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa
nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo
kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye
nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama;
lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya
silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.
Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na
mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment