“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Alhamisi, Machi 16, 2023
Juma la 3 la Kwaresima
Yer 7:23-28;
Zab 95:1-2, 6-9;
Lk 11:14-23
JE, TUME NYAMAZISHWA KUHUBIRI INJILI?
Leo, katika Injili Yesu analaumiwa kwa kutoa pepo kwa kutumia mkuu wa pepo.
Wapinzani wa Yesu walishindwa kuona kidole cha Mungu ndani ya Yesu kwa huruma
yake kwa wagonjwa. Hali hii inaonesha wazi kutokuamini kwa Mafarisayo na
viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ni Masiha. Injili ya leo inaongeleo mtu ambaye
alikuwa bubu kwasababu ya pepo. Wakati pepo alivyotolewa na Yesu, huyu mtu
aliyekuwa bubu alianza kuongea, watu wakashangaa sana. Ni hakika kwamba huyu
pepo alikuwa amemshika huyu mtu kiasi kwamba alikandamizwa kabisa mpaka
akashindwa kuongea. Baada ya kuwekwa huru kutoka katika huyu pepo, ana anza
kuongea kwa uhuru.
Ingawaje hatuwezi kuhisi uwepo wa pepo katika hali kama hii, lakini katika
hali fulani tunakutana na ukandamizaji kama wa huyu pepo wa kutufanya tubaki
kimya. Yule muovu anajaribu kutuogopesha kiasi kwamba tunakuwa waoga kutangaza
Injili kwa uhuru na kwa uaminifu, na kwa jinsi Mungu anavyopenda ujumbe wake
uwafikie watu. “pepo wa ububu” anaweza kututawala, kutuchanganya au kutujaza
hofu fulani wakati muda umefika wa kushirikisha Imani yetu na wengine. Ingawaje
ni vigumu kuanguka moja kwa moja mikononi mwao, lakini mara nyingi tunajaribiwa
kila mara na wao. Yesu ana nguvu kamilifu juu ya pepo wa aina zote, yeye hasiti
kuwanyamazisha pepo hao kama ukimruhusu. Yesu anataka kutuweka huru ili tuweze
kuongea kwa kuhubiri neno lake la upendo bila kujibakiza ili wengine waweze
kumfahamu yeye na upendo wake mkamilifu. Mwache yeye akutumie kama moja ya
chombo cha ukweli na upendo.
Sala: Bwana, wakati mwingine naingiwa na hofu na kuwa kimya na kushindwa
kutangaza neno lako vizuri kwa wale wahitaji. Wakati mwingine nahisi kama
nimefungwa kinywa kuongea, au kuchanganyikiwa niseme nini. Bwana naomba
unifungue kinywa changu niweze kuongea, Bwana wangu, ili niweze kuwa chombo
chako kitakatifu cha neno lako na kwa ujasiri na uaminifu niweze kutangaza neno
lako kwa wote walio wahitaji. Yesu, nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment