MASOMO YA MISA, MACHI 14, 2023
JUMANNE, JUMA LA 2 LA KWARESIMA
SOMO 1
Dan. 3:25, 34-43
Ndipo Azaria akasimama akasali hivi, akifumbua
kinywa chake katikati ya moto na kusema:
Usituache kabisa, kwa ajili ya jina lako, wala
usilitangue agano lako na kutuondolea rehema zako, kwa ajili ya Ibrahimu
umpendaye, na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako, na Israeli mtakatifu wako kama
nyota za mbinguni na kama mchanga wao pwani. Maana sisi, Ee Bwana, tumekuwa
duni kuliko mataifa yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa sababu
ya dhambi zetu. Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi; hakuna dhabihu
wala kafara wala sadaka wala uvumba; wala mahali pa kukutolea dhabihu na kuona
rehema.
Lakini kwa moyo uliovunjika na kwa roho
nyenyekevu tukubaliwe nawe, na sadaka yetu iwe machoni pako leo kama dhabihu za
kondoo waume na ng’ombe, na kama kondoo wanono elfu kumi. Nasi tukufuate kwa
unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika.
Na sasa tunakufuata kwa moyo wote; tunakucha na
kuutafuta uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya fadhili zako,
sawasawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya maajabu yako, na
kulitukuza jina lako, Ee Bwana.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 25:4-9 (K) 6
(K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili
zako.
Ee Bwana unijulishe njia yako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha. (K)
Ee Bwana kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,
Wala maasi yangu.
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K)
Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)
SHANGILIO
Yn. 11:25, 26
Mimi ndimi ufufuo na uzima, asema Bwana; Yeye
aniaminiye mimi, hatakufa kabisa na milele.
INJILI
Mt. 18:21-35
Petro alimwendea Yesu akamwambia, Bwana, ndugu
yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia,
Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na
mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya,
aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana
wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo,
ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana,
nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia,
akamfungua, akamsamehe ile deni.
Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli
wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, Nilipe
uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi akisema, Nivumilie,
nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata
atakapoilipa ile deni.
Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka,
walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo
bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nimekusamehe wewe deni ile
yoe, uliponisihi; nawe pia haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi
nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapolipa
deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi,
msiposamehekwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment