MASOMO YA MISA, MACHI 1, 2024
IJUMAA, JUMA LA 2 LA KWARESIMA
SOMO 1
Mwa. 37:3-4, 12-13, 17-28
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote,
maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa
baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, na hawakuweza kusema
naye kwa amani.
Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao
huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo
katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao.
Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko
Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shuri juu yake
ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja.
Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama
mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. Reubeni akasikia akamwokoa
katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, Msimwage damu;
mtupeni katika birika iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika
mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake,
wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa
katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula
chakula.
Wakainua macho yao, wakaona, msafara wa
Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na
manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa
nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? haya, na tumwuze kwa hawa
Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu.
Ndugu zake wakakubali.
Wakapita wafanyabiashara Wamidiani; basi
wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika wakamwuza Yusufu kwa
Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 105:16-21 (K) 5
(K) Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.
Akaiita njaa iijilie nchi,
Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
Alimpeleka mtu mbele yao,
Yusufu utumwani. (K)
Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
Akatiwa katika minyororo ya chuma.
Hata wakati wa kuwadia neno lake,
Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)
Mfalme alituma watu akamfungua,
Mkuu wa watu akamwachia.
Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)
SHANGILIO
Yn. 3:16
Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata
akamtoa Mwanawe wa pekee; Kila mtu amwaminiye huwa na uzima wa milele.
INJILI
Mt. 21:33-43; 45-46
Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa
watu, Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda
shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake,
akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa
karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale
wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu
wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza,
wakawatenda vile vile.
Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema,
Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana
wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake. Wakamkamata,
wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa
shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, Ataangamiza vibaya
wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa
matunda kwa wakati wake.
Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika
maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno
hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Kwa sababu hiyo nawaambia,
Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, linguine lenye kuzaa
matunda yake.
Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia
mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata
waliogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment