MASOMO YA MISA, FEBRUARI 29, 2024
ALHAMISI JUMA LA 2 LA KWARESIMA
SOMO 1
Yer. 17:5-10
Bwana asema hivi: Amelaaniwa mtu yule
amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake
amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema;
bali atakaa jangwani palipo na ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na
watu.
Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, ambaye
Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao
mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake
litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha
kuzaa matunda.
Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una
ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, Bwana, nauchunguza moyo,
navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya
matendo yake.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 1:1-4, 6 (K) 40:4
(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.
Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)
Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kw akuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
SHANGILIO
Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na
kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.
INJILI
Lk. 16:19-31
Yesu aliwaambia Mafarisayo: Palikuwa na mtu
mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula
sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake,
ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka
katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa
yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule
tajiri naye akafa, akazikwa.
Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake,
alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya
kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto
huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema
yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa
anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi
kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala
watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.
Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani
kwa baba yangu, kwa kuwaninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao
piawakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na
wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea atokaye
kwa wafu, watatubu. Akamwambia wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa
hata mtu akifufuka katika wafu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment