“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Jumatano, Februari 29, 2024
Juma la 2 la Kwaresima
Yer 18:18-20;
Zab 31:5-6,14-16;
Mt 20:17-28.
JE, TWAWEZA KUKINYWEA KIKOMBE CHA YESU?
Ni rahisi kuwa na nia nzuri, lakini hiyo inatosha? Mama mpendwa anamwambia
Yesu aagize kwamba wanawe, mmoja aketi upande wake wa kulia na mwingine upande
wa kushoto katika Ufalme wake. Lakini, ni vizuri kutambua kwamba hakujua
alichokuwa akiomba. Yesu alikuwa akienda Yerusalemu sehemu ambayo atapata
utukufu wake kwa njia ya mateso msalabani. Ni katika hali hii Yesu anawauliza
Yakobo na Yohane kama wanaweza kunywea kikombe hiki. Walikuwa wamealikwa na
Yesu kutolea maisha yao kwa sadaka kwa ajili ya upendo kwa wengine. Walipaswa
kuacha woga wote na kusema “NDIO” kwa misalaba yao wakati wakumtumikia Kristo
na utume wake.
Kumfuata Yesu sio kitu ambacho tunapaswa kufuata nusu nusu. Kama tunataka
kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu, tunapaswa kukinywea kikombe cha damu yake
takatifu ndani kabisa katika mioyo yetu na kujazwa na zawadi ili tuweze kujitoa
wenyewe hata kufikia kiwango cha kujitoa kabisa sadaka. Tunapaswa kuwa tayari
kutokuwa na kitu au kushikilia vitu, hata kama ikiwa ni sadaka kubwa. Tunaitwa
wote kuwa wafiadini wa kiroho. Hii ina maana kwamba tunapaswa kujikabidhi
wenyewe kwa Kristo na mapenzi yake na hii ina maana kwamba tutakuwa tumekufa
wenyewe kutoka katika ubinafsi wetu.
“Je, twaweza kukinywea kikombe ambacho Yesu alikinywea?” je, upendo wako
kwa Mungu na jirani waweza kuwa mkamilifu kiasi kwamba unakuwa mfiadini katika
maana halisi ya neno lenyewe? Jitambue na sema “Ndio” na kunywa katika kikombe cha damu yake
Takatifu na kila siku toa maisha yako kwa sadaka kamili. Unastahili na unaweza!
Sala: Bwana, ninaomba upendo wangu kwako na kwa wengine uongezeke kiasi
kwamba sishikilii kitu kingine nyuma yangu. Ninakuomba zawadi ya damu yako
Takatifu iwe nguvu katika safari hii ili niweze kuiga sadaka yako kamili ya
upendo. Yesu nakumini wewe. Amina
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki:
see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment