MASOMO YA MISA, FEBRUARI 4, 2023
JUMAMOSI, JUMA LA 4 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Ebr. 13:15 – 17, 20 – 21
Kwa njia yake Yesu tumpe Mungu dhabihu ya sifa
daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake. Lakini msisahau kutenda
mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu.
Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea;
maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili
kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.
Basi, Mungu wa Amani aliyemleta tena kutoka kwa
wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu
Yesu, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya
mapenzi yake; naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo;
utukufu una yeye milele na milele. Amina.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 23 (K)
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa
na kitu.
Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza,
Hunihuisha nafsi yangu. (K)
Aliniongoza katika njia za haki kwa ajili ya
jina lake.
Naam, nijapopita katika ya bonde la uvuli wa
mauti,
Sitaogopa mabaya,
Kwa maana Wewe upo pamoja nami.
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
Waandaa meza mbele yangu
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)
Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:105
Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa
njia yangu.
Aleluya.
INJILI
Mk. 6:30-34
Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa
habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia,
Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike
kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwako
nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu
wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka
miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu,
akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza
kuwafundisha mambo mengi.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Krist0.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment