MASOMO YA MISA, FEBRUARI 3, 2023
IJUMAA, JUMA LA 4 LA MWAKA
SOMO 1
Ebr. 13:1 – 8
Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili
wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.
Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao
wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mliavyo katika mwili.
Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe
safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia
ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye ymwenyewe
amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema,
Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza,
waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao,
iigeni Imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 27:1, 3, 5, 8 – 9 (K) 1
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.
Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? (K)
Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea
Hata hapo nitatumaini. (K)
Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya,
Atanisitiri katika sitara ya hema yake,
Na kuniinua juu ya mwamba. (K)
Bwana, uso wako nitautafuta.
Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu usinitupe. (K)
SHANGILIO
Zab. 130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake
nimelitumainia.
Aleluya.
INJILI
Mk. 6:14-29
Mfalme Herode alisikia habari; kwa maana jina
lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohane Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa
hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine
walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia,
alisema, Yohane mwenyewe alikuwa amefufuka.
Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu,
akamkamata Yohane, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu
yake; kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohane alimwambia Herode, Si halali kwako
kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua,
asipate. Maana Herode alimwogopa Yohane; akimjua kuwa ni mtu wa haki,
mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa
akimsikiliza kwa furaha.
Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode,
sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na
watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia,
akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia
yule kijana, Niombe lolote utakalo nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi
akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohane
Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka
unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji.
Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya
viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara
mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi, akaenda, akamkata
kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana,
naye yule kijana akampa mamaye.
Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda,
wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment