Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, FEBRUARI 20, 2023


MASOMO YA MISA, FEBRUARI 20, 2023
JUMATATU, JUMA LA 7 LA MWAKA, WA KANISA


SOMO 1
Ybs. 1:1 – 10

Hekima yote yatoka kwa Bwana, nayo yakaa kwake hata milele. Nani awezaye kuhesabu mchanga wa habari na matone ya mvua na siku za milele? Nani awezaye kutafuta kimo cha mbingu na upana wa dunia na kina cha bahari?

Hekima iliumbwa kabla ya vitu vyote, na ufahamu wa busara tangu milele. Nani aliyefunuliwa shina la hekima? Nani aliyejua mashauri yake merevu?

Yuko mmoja aliye na hekima, naye yu wa kuogopwa sana, ameketi katika kiti chake cha enzi.

Bwana ndiye aliyeiumba na kuiona na kuihesabu, na kumwaga juu ya kazi zake zote. Ina wote wenye mwili kama aitoavyo, na wale wampendao amewapa kwa wingi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 93:1 – 2, 5 (K) 1

(K) Bwana ametamalaki, amejivika adhama.

Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
Bwana amejivika, na kujikaza nguvu. (K)

Naam, ulimwengu umethibitika isitikisike;
Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani;
Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)

Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako,
Ee Bwana, milele na milele. (K)



SHANGILIO
Zab. 27:11

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unifundishe njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.



INJILI
Mk. 9:14-29

Yesu na Petro na Yakobo na Yohane walipowafikia wanafunzi, waliona makutano mkuu wakiwazunguka, na waandishi wakijadiliana nao; mara mkutano wote walipomwona walishangaa, wakamwendea mbio, wakamsalimu. Akawauliza, Mnajadiliana nini nao? Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu; na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze. Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Mleteni kwangu.

Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini; akagaagaa. Akitokwa na povu. Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, tangu utoto. Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwamngamize; lakini ukiweza neno lolote, utuhurumie, na kutusaidia. Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye. Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu. Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua; naye akasimama.

Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lolote, isipokuwa kwa kuomba.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment