MASOMO YA MISA,
FEBRUARI 14, 2023
JUMANNE, JUMA LA 6 LA MWAKA WA KANISA
KUMBUKUMBU YA WAT. SIRILI (Mtawa) NA METODI
(Askofu)
SOMO 1
Mwa. 6:5 – 8, 7:1 – 5, 10
Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni
makubwa duniani na kwamba kila kusudi analoliwaza moyoni mwake ni baya tu
sikuzote. Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika
moyo. Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi;
mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya
kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.
Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako
yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika
kizazi hiki. Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke;
na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke. Tena katika ndege wa
angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote.
Kwa maana baada ya siku saba nitainyesha dunia mvua, siku arobaini mchana na
usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wan chi nitakifutilia
mbali. Nuhu akafanya kama vile Bwana alivyomwamuru.
Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika
yakawa juu ya nchi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 29:1 – 4, 9 – 10, (K) 11
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa Amani.
Sauti ya Bwana, enyi wana wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu. (K)
Sauti ya Bwana I juu ya maji,
Bwana yu juu ya maji mengi
Sauti ya Bwana ina nguvu,
Sauti ya Bwana ina adhama. (K)
Sauti ya Bwana yawazalisha ayala,
Na ndani ya hekalu lake wanasema wote, Utukufu.
Bwana aliketi juu ya Gharika;
Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)
SHANGILIO
Zab. 25:4 – 5
Aleluya,
aleluya,
Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe
mapito yako.
Aleluya.
INJILI
Mk. 8:14 – 21
Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate,
wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, Angalieni,
jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa
wao, kwa kuwa hawana mikate.
Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona
mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo
yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki?
Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu
vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale
elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba.
Akawaambia, Hamjafahamu bado?
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment