DOMINIKA YA 6 YA MWAKA A
WIMBO WA MWANZO:
Zab. 31:2 – 4
Uwe kwangu mwamba wa nguvu, nyumba yenye maboma
ya kuniokoa. Ndiwe genge langu na ngome yangu; kwa ajili ya jina lako
uniongoze, unichunge.
SOMO 1
YbS. 15:15 – 20
Ukipenda utazishika amri zake, na kutenda amini
ni shauri lako. Ameweka mbele yako moto na maji; utanyosha mkono wako
uchaguavyo. Mbele ya mwanadamu upo uzima na muti, naye atapewa apendavyo. Mradi
hekima ya Bwana yatosha, Mkuu mwenye uweza hutazama vyote. Macho yake ni juu
yao wamchao, naye atapeleleza kila kazi ya watu. Hakumwamuru mtu yeyote awe
asi, wala kumruhusu atende dhambi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 118:1 – 2, 4 – 5, 17 – 18, 33 – 34 (K) 1
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.
Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote. (K)
Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
Ningependa njia zangu ziwe thabiti,
Nizitii amri zako. (K)
Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami italitii neno lako.
Unifumbue macho yangu niyatazame
Maajabu yatokayo katika sheria yako. (K)
Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako,
Nami nitaishika hata mwisho.
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote. (K)
SOMO 2
1Kor. 2:6 – 10
Iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si
hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali
twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu
aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kuitawala dunia hii
hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa
utukufu; lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio
halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu).
Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.
Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata
mafumbo ya Mungu.
SHANGILIO
Yn. 14:6
Aleluya, aleluya.
Mimi ndimi Njia, na Ukweli, na Uzima, asema
Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.
INJILI
Mt. 5:17:37
Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au
manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia,
Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukata moja ya torati
haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika
hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika
ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa
mkubwa katika ufalme wa mbinguni.
Mwaana nawaaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi
hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa
mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua itampasa
hukumu. Bali mimi nawaambieni, kila amwonaye ndugu yake hasira itampasa hukumu;
na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa
jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya
kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende
zako, ukapatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patina na
mshitaki wako upesi wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije
akakupeleka kwa kadhi na kadhi akakupeleka
kwa askari, akatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata
uishe kulipa senti ya mwisho.
Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi
nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye
moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling’oe ulitupe mbali nawe;
kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe
katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe;
kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee, wala mwili wako mzima usitupwe
katika jehanum. Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka;
lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya
uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini. Tena
mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usizuru, ila mtimizie Bwana nyapo zako;
lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti
cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala
kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako,
maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe
Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment