“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya kila Jumapili
Jumapili, Februari 12, 2023
Dominika ya 6 ya Mwaka A wa Kanisa
YbS 15:16-21;
Zab 118:1-2, 4-5, 17-18, 33-34;
1Kor 2:6-10;
Mt 5:17-37
KUSHIKA SHERIA!
Mungu anatuita sio katika maisha ya maadili tu, lakini katika hali ya
kuishi ya juu zaidi. Tunatembea kuelekea ukamilifu kwa kujitahidi daima
kuchagua kufanya mazuri. Katika hali ya asili sisi sio wakamilifu, lakini Mungu
anatuita tutafakari jinsi tunavyo ishi na kutambua ni kipi kimeenda vibaya na
kipi kimeenda vizuri. Kwa kutafakari maisha yetu kwa kupitia njia ya Imani
maisha yetu yanakuwa katika hekima. Yesu anatufundisha dini ambayo itatufanya
ikuwa ndani yetu na kuwa sehemu ya maisha yetu.
Somo la kwanza linatualika tufanye kila jitihada ya kufanya uchaguzi sahihi
katika maisha. Yoshua bin Sira anatangaza kwamba amri za Mungu zina nguvu ya
kuokoa. Musa aliwaambia watu alivyokuwa karibu na mto Yordani kwamba anawapa
nafasi yakuamua: maisha na mafanikio, kifo na maangamizi. Uchaguzi ulikuwa wao
kuamua. Yoshua bin Sira sasa anawaambia watu, akisisitiza ujumbe ule wa Musa
kwamba Mungu ameweka mbele yao moto na maji, maisha na kifo, mema na mabaya.
Wanatusukuma nasi tufanye uchaguzi sahihi kwa kusema kwamba macho ya Mungu huwaelekea
wale wenye kutenda mema. Ni ujumbe mzito kwetu kwamba hatuwezi kufuta mawazo
yetu na matendo yetu kutoka kwa Mungu.
Injili ya Mathayo kwa asili iliandikwa kwa ajili ya Wayahudi Wakristu,
inaweza kuonekana kama maneno ya kufariji kwao. Mathayo daima amekuwa akirejea
Agano la Kale kuwaonesha kuwa maisha ya Yesu hajaja kuvunja sheria za zamani za
Wayahudi bali ni mwendelezo wa yote ambayo yalitabiriwa na manabii hapo zamani.
Maisha na mafundisho ya Yesu hayapaswi kuonekana kama ni dini mpya, maisha ya Yesu
ni maisha ya asili ya habari ya Ukombozi. Anawahakikishia wasomaji wake kwamba
Yesu hakuja kutengua Sheria bali amekuja kuikamilisha. Kwa hiyo, sheria bado
ina nafasi yake na hivyo haitatupwa mbali hadi pale itakapo timiza jukumu lake.
Kwasababu kwa Yesu, maana halisi ya sheria inaweza kufupishwa kwa neno moja
“heshima”. Heshima kwa Mungu, kwa jina lake, kwa siku yake, heshima kwa wazazi,
heshima kwa uhai, utu, heshima kwa ukweli na heshima kwa jina la mtu na
hatimaye heshima kwa nafsi. Kwa maneno mengine sheria yote inahitimishwa kwa
‘heshima kwa Mungu’ na ‘heshima kwa nafsi” na jirani. Kwasababu heshima hii
haijalimbikizwa katika visheria vidogo na miiko bali imejibeba katika amri ya
mapendo: Upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani. Yesu hakutambulisha sheria mpya
bali alitambulisha njia mpya yakufikiria na kuelewa sheria. Hakutengua sheria
wala kubadili bali alienda mbele zaidi ya kile kinacho hitaji. Kwasababu kwa
Yesu, hali ya nje tu ya kushika sheria haitoshi. Kuwa mfuasi wa Yesu ni vizuri
kutambua sheria iliojengwa katika mapendo. Kushika sheria bila mapendo ni sawa
na kuwa na mwili bila roho. Ndio maana anawaambia wafuasi wake kwamba fadhila
zao zisipo zidi zile za Mafarisayo na Waandishi, hawataingia katika Ufalme wa
Mungu.
Ili kuwafanya wafuasi wake waelewe mafundisho yake, Yesu aliwapa mifano
sita mizito na katika injili ya leo tuna minne, tuna kuhusu: hasira, uasherati,
talaka na kiapo. Anasema wazi kwamba haitoshi tu kushika ambacho sheria
inatuambia bila kutenda fadhila zinazo ambatana nazo. Kwa Yesu, hakuwezi kuwa
na utengano kati ya uhusiano wetu na Mungu na watu. Mkristo anapaswa kumpata
Mungu kwa watu wote na katika uumbaji.
Sala: Bwana, nifanye niwe safi moyoni. Nifanye niweze kuwa mtu mwaminifu na
mwenye kujali utu. Ninaomba ukweli ulio uweka ndani ya moyo wangu uweze kuwa
msingi wa matendo yangu na maneno yangu. Ninaomba niongee nikiwa na dhamiri
safi kila wakati nikiongea ulichonipa niongee. Yesu, nakumini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment