MASOMO YA MISA, JANUARI 31, 2023
JUMANNE JUMA LA 4 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA MT. YOHANE BOSKO, PADRE
SOMO 1
Ebr. 12:1 – 4
Kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la
mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo
kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele
yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza Imani yetu; ambaye
kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau
aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakari
sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya
nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu. Hamjafanya vita hata
kumwagika damu, mkishindana na dhambi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 22:25 – 27, 29 – 31 (K) 26
(K) Wanaokutafuta, Ee Bwana, watakusifu.
Nitaziondoa nadhiri zangu mbele zao wamchao.
Wapole watakula na kushiba,
Wamtafutao Bwana watamsifu;
Mioyo yenu na iishi milele. (K)
Miisho yote ya dunia itakumbuka,
Na watu watamrejea Bwana,
Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu,
Humwinamia wote washukao mavumbini. (K)
Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,
Wazao wake watamtumikia.
Zitasimuliwa habari za Bwana,
Kwa kizazi kitakachokuja,
Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake,
Ya kwamba ndiye aliyeyafanya. (K)
SHANGILIO
Yn. 17:17
Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa
ile kweli.
Aleluya.
INJILI
Mk. 5:21 – 43
Yesu alipokwisha kuvuka kurudia ng’ambo katika
kile chombo, wakamkusanyikia mkutano mkuu; naye alikuwa kando ya bahari. Akaja
mtu mmoja katika wakuu wa sinagogi, jina lake Yairo; hata alipomwona, akaanguka
miguuni pake, akimsihi sana, akisema, Binti yangu mdogo yu katika kufa;
nakuomba uje, uweke mkono wako juu yake, apate kupona, na kuishi. Akaenda
pamoja naye. Mkutano mkuu wakamfuata, wakimsong-songa.
Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa
miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi,
amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake
ilizidi kuwa mbaya; aliposikia habari za Yesu, alipita katiak mkutano kwa
nyuma, akaligusa vazi lake; maana, alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu,
nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, anaye akafahamu mwilini mwake
kwamba amepona msiba ule.
Mara yesu, ahali akifahamu nafsi ni mwake kwamba
nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi
yangu? Wanafunzi wake wakambwambia, Je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa,
nawe wasema, Ni nani aliyenigusa? Akatazama pande zote ili amwone yule
aliyelitenda neno hilo. Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka,
akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote. Akamwambia,
Binti, Imani yako imekuponya, enenda zako kwa Amani, uwe mzima, usiwe na msiba
wako tena.
Hata laipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka
kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi
kumsumbua mwalimu? Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia
mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu. Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila
Petro, na Yakobo, na Yohane nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa
sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu.
Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa,
bali amelala tu. Wakamcheka sana.
Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa
babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani
alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi;
tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda;
maana laikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao
mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment