MASOMO YA MISA, JANUARI 27, 2023
IJUMAA, JUMA LA 3 LA MWAKA
SOMO 1
Ebr. 10:32 – 39
Zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha
kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; pindi mlipotwezwa kwa
mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo. Maana
mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha
kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema
zaidi, idumuyo. Basi msiutupe ujasiri wetu, kwa maana una thawabu kuu. Maana
mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile
ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.
Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa Imani; naye akisitasita, roho yangu haina
furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo
miongoni mwa hao walio na Imani ya kutuokoa roho zetu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 37:3 – 6, 23 – 24, 39 – 40 (K) 39
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.
Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako. (K)
Umkabidhi Bwana njia yako pia umtumaini
Naye atafanya;
Ataitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri. (K)
Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana,
Naye aipenda njia yake.
Ajapojikwaa hataanguka chini,
Bwana humshika mkono na kumtegemeza. (K)
Wokovu wa wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa,
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)
SHANGILIO
1Thes. 2:13
Aleluya, aleluya,
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la
wanadamu, bali kama neno la Mungu.
Aleluya.
INJILI
Mk. 4:26-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa Mungu,
mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka,
usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa
yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda
yakiiva, mara aupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika.
Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu?
Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika
nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha
kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa;
hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake.
Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema
nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema
nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment