MASOMO YA MISA, JANUARI 24, 2023
JUMANNE, JUMA LA 3 LA MWAKA
KUMBUKUMBU YA MT. FARANSISKO WA SALES (ASKOFU NA
MWALIMU WA KANISA)
SOMO 1
Ebr. 10:1 – 10
Kwa kuwa torati ni kivuli cha mema yatakayokuwa,
wala si sura yenyewe ya mambo hayo kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka
daima haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao. Kama ndivyo, je! Dhabihu
hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja,
wasingejiona tena kuwa na dhambi? Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la
dhambi kila mwaka. Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.
Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema.
Dhabihu na toleo hukutaka, lakini mwili uliwekea
tayari; sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; ndipo
niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye
mapenzi yako, Mungu.
Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka
za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendwazwa nazo
(zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja
niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili.
Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara
moja tu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 40:1, 3, 6 – 7, 10 (K) 7, 8
(K) Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja,
kuyafanya mapenzi yako.
Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu.
Akatia wimbo mpya kinywani mwangu
Ndio sifa zake Mungu wetu. (K)
Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)
Nimehubiri habari za haki
Katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu;
Ee Bwana, unajua. (K)
Sikusitiri haki yako moyoni mwangu,
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa. (K)
SHANGILIO
Yak. 1:21
Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno la Mungu lililopandwa
ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.
INJILI
Lk. 10:1-9
Bwana aliweka wengine, sabini, akawatuma wawili
wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe.
Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni
Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni; angalieni,
nawatuma kama wana-kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala
viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni
kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu
itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo
hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira
wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wowote
mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni
wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment