MASOMO YA MISA, JANUARI 23, 2023
JUMATATU, JUMA LA 3 LA MWAKA
SOMO 1
Ebr. 9:15, 24 – 28
Kristo ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti
ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao
walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele.
Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu
palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia
mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba
ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila
mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu
kuwekwa msingi wa ulimwengu, lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa
nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile
watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo
naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi;
atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1 – 6 (K) 1
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu
wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K)
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi;
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele ya mfalme, Bwana. (K)
SHANGILIO
2Tim. 1:10
Aleluya, aleluya,
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti, na
kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya.
INJILI
Mk. 3:22-30
Waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema,
Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. Yesu akawaita akawaambia kwa
mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi
yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake,
nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake,
akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya
nyumba ya mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye
nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake.
Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa
wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho
Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakauwa ana dhambi ya milele; kwa vile
walivyosema, Ana pepo mchafu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment