Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JANUARI 21, 2023


MASOMO YA MISA, JANUARI 21, 2023
JUMAMOSI LA 2 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA MT. AGNES (BIKIRA NA SHAHIDI)


SOMO 1
Ebr. 9:2 – 3, 11 – 14

Hema ilitengenezwa, ile ya kwanza, mlimokuwa na kinara cha taa, na meza, na mikate ya Wonyesho; ndipo palipoitwa, Patakatifu. Na nyuma ya pazia la pili, ile hema iitwayo Patakatifu pa patakatifu.

Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 47:1 – 2, 5 – 8

(K) Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
na Bwana kwa sauti ya baragumu.

Enyi watu wote pigeni makofi,
Mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe.
Kwa kuwa Bwana Aliye juu, mwenye kuogofya,
Ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. (K)

Mungu amepaa kwa kelele za shangwe,
Bwana kwa sauti ya baragumu.
Mwimbieni Mungu, naam, imbeni,
Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. (K)

Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote,
Imbeni kwa akili.
Mungu awamiliki mataifa,
Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu. (K)



SHANGILIO
Kol. 3

Aleluya, aleluya,
Neno la Kristu likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote; mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.
Aleluya.



INJILI
Mk. 3:20-21

Yesu aliingia nyumbani na mkutano wakakusanyika tena, hao wao wenyewe wasiweze hata kula mkate. Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment