MASOMO YA MISA, JANUARI 20, 2023
IJUMAA, JUMA LA 2 LA MWAKA WA KANISA
SOMO 1
Ebr. 8:6 – 13
Kuhani wetu sasa amepata huduma iliyo bora
zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi
zilizo bora. Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi
isingalitafutwa kwa lile la pili. Maana, awalaumupo, asema, Angalia, siku
zinakuja, asema Bwana, nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda
agano jipya; halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, katika siku
ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu
hawakudumu katika agano langu, Mimi nami sikuwajali, asema Bwana.
Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba
ya Israeli baada ya siku zile asema Bwana; nitawapa sheria zangu katika nia
zao, na katika mioyo yao nitaziandika; nami nitakuwa Mungu kwao, nao watakuwa
watu wangu. Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, na kila mtu na ndugu
yake, akisema, Mjue Bwana; kwa maana wote watanijua, tangu mdogo wao hata
mkubwa wao. Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, na dhambi zao sitazikumbuka
tena. Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu.
Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 85:7, 9 – 13 (K)
(K) Fadhili na kweli zimekutana.
Ee Bwana, utuonyeshe rehema zako,
Utupe wokovu wako.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu. (K)
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)
SHANGILIO
Efe. 1:17, 18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya
hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
INJILI
Mk. 3:13-19
Yesu alipanda mlimani, akawaita aliowataka
mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na
kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo. Akawaweka wale
Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro; na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na
Yohane nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo;
na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa
Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment