ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Ijumaa, Januari 20, 2023
Juma la 2 la Mwaka wa Kanisa
Ebr 8: 6-13;
Zab 85: 8, 10-14;
Mk 3: 13-19
KUELEKEA MLIMANI!
Leo Yesu anawaita wale aliotaka kujenga nao jumuiya moja. Yeye aliwateua
kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye na kwamba apate kuwatuma kuhubiri na
kuwapa mamlaka ya kuwafukuza pepo. Yeye anawakaribisha katika uhusiano maalum
na yeye mwenyewe ili aweze kuwatuma,na walete mabadiliko katika dunia hii.
Kitu kimoja muhimu ni kwamba Yesu yupo na wanafunzi wake “mlimani”. Jambo
hili linaonesha au kutoa funzo/alama muhimu. Uwepo wa mitume kuhubiri na kutoa
pepo unaanza tu mara baada ya Yesu kwenda mlimani nao. Kwanini anafanya hivyo
mara baada tu ya kuwaita mlimani?
Mlima ni alama ya safari yetu kumwelekea Mungu. Ni alama kwamba tunapaswa
kupanda kumwelekea Yeye. Na inaonyesha kwamba tunaweza kwenda kufanya mapenzi
ya Mungu tu pale ambapo tumeshaenda kumuona na kukutana nae. “Mlima” tunaoitwa
kuupanda ni “sala”. Tunapaswa kupanda mlima kila siku kwenda kukutana na Bwana,
kumtafuta katika maisha yetu kwa maisha ya ndani na kujikabidhi kwake. Yesu
anatuita sisi kwake pale ambapo yupo anatusubiri ili tuweze kuwa naye
tukifurahi uwepo wa utukufu wake. Tusipo enda kukutana na Yesu katika mlima,
itakuwa vigumu kutimiza utume wake mtakatifu. Tutakuwa tumepungukiwa katika
kuleta huruma na mapendo ulimwenguni. Yesu anakupa nafasi ya kumfuata katika
mlima wa sala. Mjibu mwaliko wake ili aweze kukutuma kutimiza amri yake ya mapendo.
Sala: Bwana, ninakubali mwaliko wako wa upole wa kwenda mlima wa Imani na
sala. Natamani kukutafuta na kuwa nawe. Ninapo kutana nawe katika sala, nipe
neema ninazo hitaji ili niweze kwenda ulimwenguni kutimiza mapenzi yako. Yesu,
nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment