Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JANUARI 19, 2023


MASOMO YA MISA, JANUARI 19, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 2 LA MWAKA WA KANISA

SOMO 1
Ebr. 7:25 – 8:6

Yesu aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.

Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengi, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi zao hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele.

Basi, aktika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu. Maana kila kuhani mkuu huwekwa ilia toe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima huyu naye awe na kitu cha kutoa. Kama angekuwa juu ya nchi, asingekuwa kuhani; maana wako watoao sadaka kama iagizavyo sheria; watumikiao mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule ulioonyeshwa katika mlima.

Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 40: 6 – 9, 16 (K) 7,8

(K) Tazama nimekuja kufanya mapenzi yako, Ee Bwana.

Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja. (K)

Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)

Nimehubiri habari za haki, Katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu, Ee Bwana, unajua. (K)



SHANGILIO
2 Kor. 5:19

Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisha.
Aleluya.



INJILI
Mk. 3:7-12

Yesu alijitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea. Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa. Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. Akawakataza sana, wasimdhihirishe.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment