Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JANUARI 18, 2023


MASOMO YA MISA, JANUARI 18, 2023
JUMATANO, JUMA LA 2 LA MWAKA WA KANISA


SOMO 1
Ebr. 7:1 – 3, 15 – 17

Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme akambariki; ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa Amani; hana baba, hana mama, mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele.

Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki; asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo; maana ameshuhudiwa kwamba, wewe u kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 110:1 – 4 (K) 4

(K) Ndiwe kuhani hata milele kwa mfano wa Melkisedeki.

Neno la Bwana kwa Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume,
Hata niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako. (K)

Bwana atainyosha toka Sayuni fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako. (K)

Watu wako wanajitoa kwa hiari,
Siku ya uwezo wako,
Kwa uzuri wa utkatifu,
Tokea tumbo la asubuhi,
Unao umande wa ujana wako. (K)

Bwana ameapa, wala hataghairi,
Ndiwe kuhani milele hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki. (K)



SHANGILIO
Yn. 17:17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya, aleluya.



INJILI
Mk. 3:1-6

Yesu aliingia katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza; wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki. Akawaambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati. Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza. Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment