Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JANUARI 16, 2023



MASOMO YA MISA, JANUARI 16, 2023
JUMATATU, JUMA LA 2 LA MWAKA

SOMO 1
Ebr. 5:1 – 10

Kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ilia toe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Na hapana mtu alitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni.

Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye yaliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa, kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani milele kwa mfano wa Melkizedeki. Yeye siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mates ohayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii; kisha ametajwa na Mungu kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 110:1 – 4 (K) 4

(K) Ndiwe kuhani hata milele, kwa mfano wa Melkizedeki.

Bwana atainyosha toka Sayuni
Fimbo ya nguvu zako.
Uwe na enzi kati ya adui zako. (K)

Watu wako wanajitoa kwa hiari,
Siku ya uwezo wako;
Kwa uzuri wa utakatifu,
Tokea tumbo la asubuhi,
Unao umande wa ujana wako. (K)

Bwana ameapa,
Wala hataghairi,
Ndiwe kuhani hata milele,
Kwa mfano wa Melkizedeki. (K)



SHANGILIO
Lk. 8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.




INJILI
Mk. 2:18-22

Siku moja wanafunzi wake Yohane na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?

Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile. Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment