MASOMO YA MISA, JANUARI 13, 2023
IJUMAA, JUMA LA 1 LA MWAKA
SOMO 1
Ebr. 4:1 – 5, 11
Ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake,
na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi
tumehubiriwa habari njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa
halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na Imani ndani yao waliosikia.
Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, Kama
nilivyoapa kwa hasira yangu, hawataingia rahani mwangu; ijapokuwa zile kazi
zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya uolimwengu. Kwa maana ameinena siku ya
saba mahali Fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake
zote; na hapo napo, Hawataingia rahani mwangu.
Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile,
ili kwamba mtu yeyote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 78:3 – 4, 6 – 8 (K) 7
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.
Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu,
Ambayo baba zetu walituambia,
Tukiwaambia kizazi kindine
Sifa za Bwana na nguvu zake. (K)
Wasimame na kuwaambia wana wao,
Wamwekee Mungu tumaini lao,
Wala wasiyasahau matendo ya Mungu,
Bali wazishike amri zake. (K)
Wasiwe kama baba zao,
Kizazi cha ukaidi na uasi,
Kizazi kisichojitengeneza moyo,
Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu. (K)
SHANGILIO
Yn. 17:17
Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa
ile kweli.
Aleluya.
INJILI
Mk. 2:1-12
Baada ya siku Yesu akaingia tena Kapernaumu.
Ikasikiwa ya kwamba Yesu alikuwa nyumbani. Wakusanyika watu wengi, isibaki
nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake. Wakaja watu wakimletea mtu
mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia
kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja
wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.
Naye Yesu, alipoiona Imani yao, akamwambia yule
mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi yay a waandishi
walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi?
Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?
Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba
wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu?
Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema,
Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa
Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye
kupooza), Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende nyumbani kwako. Mara
akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu
wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora
- Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are
published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings
are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment