Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

WOTE WANAALIKWA KWENYE MEZA YA YESU!


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Ijumaa, Desemba 9, 2022
Juma la 2 la Majilio

Isa 48:17-19;
Zab 1:1-4, 6;
Mt 11:16-19


WOTE WANAALIKWA KWENYE MEZA YA YESU!


Yesu katika Maandiko Matakatifu anakaa katika meza ya undugu na waliotengwa, waovu, kahaba, waliovunjika moyo, maskini, wajane, na wote waliotengwa na jamii. Mathayo na Zakayo walioonekana waovu na watoza ushuru, walikuja kumfahamu Mungu kupitia Yesu na wakajiunga katika utume wake. Zaidi ya “kahaba” mmoja waliweza kutambua utu wao na uzuri wao wandani kwa njia ya Yesu, na wakajiunga na utume wake. Zaidi ya mjane mmoja walitambua utakatifu wa Yesu na kufuata utume wake.Maskini waligundua utajiri wa hali ya juu kwa Yesu na wakafuata mafundisho yake. Ni zaidi ya Mjane mmoja aliyetambua ulinzi zaidi kwa Yesu na kufuata utume wake. Wote waliopondeka moyo kwasababu ya magonjwa yao na kutokujiweza kwao, kati yao walio onekana kama laana na adhabu kwasababu ya dhambi zao, walipata uponyaji kwa Yesu na kumfuata. Mwizi yule katika msalaba maisha yake ya milele yalibadilika na kumfuata katika paradise ya milele. Yesu alikula, kunywa, kucheka, na kuwapenda walio onekana wabaya katika jamii na kula nao mezani. Kwa hakika bado anawapenda. Kwa Yesu tunakumbushwa ni upendo wa hali ya juu unao andaa moyo ili kukubali, sio malalamiko, mapendo ya kweli yanatarajia kulenga kubadilisha na sio kuhukumu.

Yesu anaeleza kwamba yeye pamoja na Yohane Mbatizaji walituhumiwa uongo kuwa wadhambi. Yohane kwa mfano, alifunga sana, kitu ambacho ni fadhila. Lakini Mafarisayo walitafsiri vibaya kuwa ni kazi ya muovu. Yesu alitumia muda mwingi akiwa mgeni katika nyumba za watu, wakamwita mlafi na mlevi. Wakati mtu alivyofanya vizuri, walijaribu kubadili ukweli na kujaribu kupotosha uhalisia. Hii mara nyingi inafanyika kwasababu ya chuki au wivu. Hali hii inatupa muda wa kujitafiti na kujichunguza ni kwa jinsi ghani tulivyo waaminifu na wa kweli kuhusu uhusiano wetu na wengine, uhusiano wetu kati yetu.

Tujichunguze wenyewe jinsi tunavyo waangalia na kuwachukulia ndugu zetu walio karibu nasi, na zaidi jinsi tunavyoongea kuhusu wao. Kama ukijiona mwenyewe ukianguka katika hali ya wivu na chuki, ni vizuri kujikabidhi katika huruma ya Mungu ili hali hiyo isije ikazaa dhambi kubwa zaidi.

Kwa namna ya pekee tunaliombea taifa letu la Tanzania linalo adhimisha siku ya uhuru. Tunawaombea watu wake wote, Amani na furaha. Kwa maombezi ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili aliye msimamizi wa nchi yetu, atuombee daima.

Sala: Bwana, nisaidie niweze kuwaona wenzangu katika mwanga wa unyenyekevu na ukweli. Naomba unisaidie niweze kuona fadhila zao na vipaji vyao nivifurahie. Ondoa ndani mwangu wivu mbaya na chuki binafsi. Yesu nakutumainia wewe. Amina

                                    
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment