“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumatano, Desemba 7, 2022
Juma la 2 la Majilio
Kumbukumbu ya Mt. Ambrosi, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Isa 40: 25-31;
Zab 103: 1-4, 8, 10;
Mt 11: 28-30.
TUKABIDHI MIZIGO YETU TUPATE PUMZIKO KWA YESU!
Kuna hadithi maarufu ya mtu ambaye alikutana na
kijana wa kiume akiwa amembeba mtoto mlemavu mgongoni mwake. Yule mtu alitamka,
“huo uubebao ni mzigo mzito.” Yule kijana wa kiume alijibu, “Huu sio mzigo;
huyu ni mdogo wangu!” hakuna mzigo ulio mzito kama utakuwa umebebwa kwa upendo.
Yesu ametufundisha sisi nguvu ya upendo kupitia maneno yake na mifano yake.
Katika ufalme wake, dhambi hazisamehewi tu bali zinafutwa kabisa, na uzima wa
milele hutolewa kwa watu wake wote. Ni Yesu pekee anaweza kuinua mzigo wa
dhambi na uzito wa kupoteza tumaini kutoka kwetu. Yesu anatumia mfano wa nira
kuelezea ni namna gani tunaweza kubadilisha mzigo wa dhambi na kupoteza tumaini
kuwa utukufu na nira ya uhuru dhidi ya dhambi.
Kipindi cha majilio kinatukumbusha kwamba Mungu
Mwana alikuja duniani na akachukua hali ya ubinadamu wetu. Lakini ingawaje
hakutenda dhambi, yeye aliruhusu kubeba mzigo wa dhambi zetu. Ili yeye kama
Mungu, aweze kutuangalia nakutuambia kwamba anaelewa ni nini maana yake
kwasababu yeye mwenyewe amebeba mzigo huo kwa ajili yetu. Aliingia katika hali
hii kwasababu ya upendo aliokuwa nao kwetu ili atusaidie na sisi kuvumilia, kwa
furaha, tunapokumbana na maisha yetu ya kila siku.
Je, ni namna gani tunaweza kujiweka katika nira
ya mkombozi? Jibu linapatikana katika amri ‘jifunzeni kutoka kwangu’. Anatuita
tutumikie, lakini tunafanya kazi hiyo na kuhudumia kwa nguvu atukirimiazo.
Daima Yeye yupo karibu nasi kutupunguzia mizigo. Hili litafanyika kama tu
tutayakabidhi maisha yetu kwake. Mizigo inakuwa mizito na haibebeki pale tu
tunapojaribu kuichukua wenyewe, au kuimudu sisi wenyewe. Je, unauamini upendo
wa Mungu na kukubali mapenzi yake katika maisha yako?
Sala: Bwana, nakabidhi maisha yangu kwako na yote
nilio nayo kwako. Ninakubali mwaliko wako. Asante kwa huruma yako na kunijali
mimi kila wakati. Yesu nakuamini wewe. Amina
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment