MASOMO YA MISA DESEMBA 7,
2022
JUMATANO, JUMA LA 2 LA MAJILIO
KUMBUKUMBU YA MT. AMBROSI, ASKOFU NA MWALIMU WA KANISA
SOMO 1
Isa. 40:25-31
Mtanifananisha na nani, nipate kuwa sasa naye? Asema yeye
aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi;
aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza
wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali
pake.
Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia
yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu
asiiangalie? Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba
miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu
wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Haya vijana watazimia na
kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu
mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka;
watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 103:1-4,8,10 (K) 1
(K) Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Naam, vyote vilivyo ndani yangu,
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)
Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)
Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hakututenda sawasawa na hatia zetu.
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana atakuja kuwaokoa watu wake, Heri walio
tayari kumlaki.
Aleluya.
INJILI
Mt. 11:28-30
Siku ile, Yesu alijibu akasema: Njoni kwangu nyote
msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu,
mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata
raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment