“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, Desemba 18, 2022
Dominika ya 4 ya Majilio
Isa 7:10-14;
Zab 23:1-6;
Rum 1:1-7;
Mt. 1:18-24.
MUNGU PAMOJA NASI!
Watoto ni zawadi katika ndoa. Wanapo ingia katika ulimwengu wa wazazi, uhusiano wao huanza kubadilika. Watoto wanahitaji uangalizi wa hali ya juu, wanapo anza kuingia katika ulimwengu wa kawaida wa wazazi wao. Mimi na wewe tuna ulimwengu wetu, mipango yetu, na tamaa zetu ambazo hizi hatutaki ziingiliwe. Ulimwengu wa mtu kugeuzwa juu chini na mtoto inaweza kuwa ni usumbufu mkubwa sana.
Tupo leo kwenye Dominika ya 4 ya Majilio, tukitafakari jinsi ya kuingia katika fumbo la umwilisho ambalo tutaliadhimisha wakati wa Noeli. Njia moja ya kuandaa mioyo yetu na kuhisi uwepo wa juu wa Yesu akija kwetu ni kujikabidhi kwake na kukuwa katika uhusiano wetu na Mungu kwa njia ya neno lake.
Leo hii katika masomo tunaona jinsi Mungu anavyo ingia katika ulimwengu wa Ahazi, Paulo, Maria na Yosefu. Katika somo la kwanza tunamuona Mungu akiingia katika maisha ya Ahaz, na kumwambia aombe ishara ya Bwana, na alama anayotaka. Ahaz ansema hapana. Hili ni Muhimu sana. Katika tamaduni na mapokeo, Mtu hapaswi kumjaribu Mungu. Lakini hapa sasa ni Mungu anamwambia Ahaz amweke katika majaribu, lakini ahazi anasema hapana kwa Neno la Mungu na kusema ndio kwa sheria na mapokeo. Ahazi alisikia alichosema Mungu, lakini akaamua kutokufuata sauti ya Mungu. Kwa hiyo hakuna uhusiano ulioanzishwa kati yao, Ahazi anakataa kubadilika hata baada ya Mungu kuingia katika maisha yake.
Katika hali kama ya Ahaz, tunaona katika Injili Mungu akiingia katika maisha ya Yosefu na Maria. Mungu anamwambia Yosefu afanye kitu ambacho ni tofauti na sheria na Torati, kwa kumwambia amchukue Maria awe mke wake, wakati Maria ana mimba. Lakini Yosefu anatii, kinyume kabisa na Ahazi, Yosefu anasema ndio kwa Mungu, na hapana kwa sheria na Torati. Anapokea Neno la Mungu, na kufanya yalio mapenzi ya Mungu, ingawaje waweza kudhani sio hekima. Kwahiyo, anamsikiliza Mungu, anatii sauti ya Mungu, na kwa utii kabisa kufanya kile anacho mwelekeza Mungu. Hili ilikuwa ni upendo na Imani katika matendo, bila kujali jamii iliomzunguka itamfikiriaje. Neno la Mungu liliingilia maisha yake, na hivyo kushiriki katika fumbo la umwilisho kwa kuwa mume wa Maria.
Ingawaje Mama yetu Maria alikuwa mkamilifu na Mt. Yosefu alikuwa mtu wa fadhila kuu, walikuwa ni wanadamu kamili. Yosefu alikumbwa na fumbo kubwa la hali ya juu baada ya kutambua mke wake ni mjamzito. Alimtambua mke wake kama mwanamke aliyekuwa na fadhila ya pekee na utakatifu na hivyo anashangazwa na yeye kuwa na mimba. Hata hivyo baada ya Malaika kumtokea katika ndoto angeweza bado kuwa na maswali moyoni mwake ya kuuliza alivyokuwa akikumbana na hali hii. Mama yetu Maria mbarikiwa alialikwa na Mungu pia kupokea mimba kwa Imani. Jibu lake lilikuwa kamili “Na iwe kwangu kama ulivyo nena” hakuweza kuelewa na kutambua yaliokuwa yanatokea lakini alitambua ndani kabisa moyoni mwake kwamba Mungu ndiye anaye ongoza yote kwa utukufu wake. Wote wawili Maria na Yosefu ni mfano halisi wa Imani na utii kwa Mungu. Walikuwa watii wa mapenzi ya Mungu ingawaje mapenzi ya Mungu yaliwavuta karibu na fumbo la ndani kabisa na la ajabu. Walikuwa mashuhuda wa kwanza wa Mkombozi wa ulimwengu na tukio ambalo halijawahi kutokea. Wote walipokea fumbo hili na kulikubali kwa Imani.
Mt. Paulo katika barua yake kwa Warumi, anahitimisha habari njema kwa kuwaambia kwamba Kristo alizaliwa katika ukoo wa Daudi na Mwana wa Mungu. Na anaendelea kwa kusema kwamba Yesu alituletea maisha mapya na kwa njia ya neema hii inayo badili mapendo yetu, tunaletwa katika maisha mapya na kuwa na uhusiano na Mungu.
Bwana amekuja katika historia, Bwana yupo nasi katika mafumbo ya Sakramenti na Bwana atakuja tena katika utukufu. Katika kipindi hichi cha kujiandaa kwa karibu kabisa kwa kuzaliwa kwa Bwana wetu, tunajitazama ndani yake yeye aliye zawadi ya Mungu kwetu. Masiha ataingia ulimwenguni kama mtoto. Mtoto huyu atakuja katika maisha yetu, ili aweze kuwa katika mahusiano yetu. Tunapaswa kufungua maisha yetu tumpokee na atubadilishe. Tunapaswa kufungua mlango wa mioyo yetu na kumruhusu Mungu aje ndani. Kwa kufanya hivyo, tunapaswa tusikilize na kuijibu sauti ya Mungu, hata kama inakuita ufanye tofauti na jinsi watu walivyozea katika jamii. Kwa kumsikiliza Mungu na kumtii, tunaingizwa katika maisha mapya kwa kushika Imani yetu kikamilifu. Na kwa njia hiyo tutakuwa tayari kufungua moyo ili Mungu atubadili mioyo yetu kwa upendo wake.
Tutafakari pia kuhusu mwaliko wetu binafsi kutoka kwa Mungu wa kushikamana na maumbo matakatifu katika maisha yetu. Maria na Yosefu wanatupa sisi ushuhuda wa jinsi ya kushikilia mafumbo ya Mungu anayotualika tuyashiriki. Tuseme ndio kwa mapenzi ya Mungu kama hawa wachumba watakatifu walivyofanya. Isaya na Matayo wanatuambia kuhusu huyu Mungu kwamba ni Emmanueli maana yake “Mungu pamoja nasi”. Na kweli yupo kati yetu. Mungu yupo karibu nasi na katika kila hatua tunayo fanya, katika kila saa tunayoishi na kila mahali Mungu yupo nasi. Tunapomsikiliza na kumtii Mungu, yupo nasi na anatutia moyo na kutuongoza. Yupo nasi hata pale wote wanapo ondoka na kutuacha na kujitenga nasi, na anatusamehe tunapo mkosea na kumwomba msamaha.
Sala: Wapendwa Maria na Yosefu, niombeeni niweze kuwa na Imani mliokuwa nayo. Wakati maswali yanapo ikumba roho yangu, nisaidieni niweze kumjibu Mungu kwa ukarimu kama mlivyofanya. Naomba nisadiki yote aliosema Mungu kwa kuwaiga ninyi. Yesu nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2022 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment